Harmonize Atangaza Ujio wa Konde Gang Radio na TV

[Picha: Harmonize Instagram]

Mwandishi: Brian Sikulu

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki nyota kutoka Tanzania Harmonize ametangaza kukamilika kwa vituo vya Konde Gang FM na Konde Gang TV. Harmonize ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa Konde Music Worldwide alichapisha tangazo hilo kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Harmonize hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na vituo hivyo. Hakutaja tarehe kamili ya uzinduzi au mitabendi ambazo vituo hivyo vitakuwa vikitumia kupeperushwa hewani.

Soma Pia: Harmonize Afichua Sababu Iliyomfanya Kuanzisha Lebo ya Konde Music Worldwide

Tayari tangazo hilo limezua gumzo mtandaoni huku wengi wa mashabiki wakijitokeza na kumpongeza. Harmonize ambaye pia anafahamika kama Jeshi kimuziki, anaonekana kufuata nyayo za bosi wake wa zamani Diamond Platnumz.

Diamond vile vile alianzisha lebo yake ya rekodi ambako alimsajili Harmonize kabla ya wawili hao kutofautiana.

Baadaya kufungua lebo yake ya Wasafi, Diamond alizindua vituo vya Wasafi FM na Wasafi TV ambavyo vilipokelewa vizuri sana na mashabiki. Harmonize yupo kwenye njia sawia na Diamond Platnumz kwani baada ya kuzindua lebo yake ya rekodi, anakwenda kuzindua vituo vyake vya redio na televisheni.

Soma Pia: Harmonize Amshauri Ibraah Kuacha Ugomvi na Wasanii Wengine Bongo

Wadau mbali mbali katika muziki wamedai kuwa uwepo wa vituo vya redio na televisheni husaidia msanii kusambaza nyimbo zake na hivyo basi kumletea mafanikio zaidi. Wengi wa mashabiki kwa sasa wanasubiri tarehe kamili ya uzinduzi wa Konde Gang FM na Konde Gang TV.

Leave your comment