Marioo Asifia Ustadi Wa Harmonize Katika Kuimba Nyimbo Za Ushairi Mzito

[Picha: Harmonize Instagram]

Mwandishi: Brian Sikulu

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Msanii wa Bongo Flava Marioo amejitokeza na kusifia ustadi wa Harmonize katika kutengeneza na kuimba nyimbo za hisia. Kupitia ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wa Instagram, Marioo alieleza kuwa mashabiki hubaki na furaha tele kila mara Harmonize anaachia ngoma yenye hisia.

Marioo alikuwa akizungumza kuhusu wimbo wa Harmonize wa Sorry ambao unaovuma sana kwa sasa.

"Konde akiingiaga anga hizi lazima mshike vichwa. Nomaa," Marioo aliandika mtandaoni.

Aliambatanisha ujumbe wake na emoji za moto na kunyoosha mikono kwa maana kuwa alikuwa ameikubali kazi ya Harmonize.

Hata hivyo, si Marioo tu aliyeikubali kazi yake Harmonize, kwani msanii Korede Bello pia alimpongeza Harmonize kuimba kwa ustadi mkubwa sana. Korede Bello alimtumia Harmonize ujumbe wa kibinafsi kupitia ukurasa wa Instagram ambapo alimsifu pia kwa wimbo huo.

Kilichowavutia watu wengi kwenye wimbo huo haikuwa ujumbe tu, bali pia namna Harmonize alivyojieleza. Msanii huyo alionekana mwenye majuto makubwa kwa kumkosea mpenzi wake wa zamani Sarah.

Hisia hazikuwepo tu kwenye mistari ya wimbo huo, bali pia kwenye sauti na matendo ya Harmonize wakati akiimba.

Cha muhimu pia kutajwa ni kuwa tofauti na ilivyo kawaida, wimbo huo haukurekodiwa studioni bali uliimbwa mbashara huku ukipeperushwa moja kwa moja mtandaoni. Upeperushaji huo ulimaanisha kuwa mashabiki walikuwa wakitazama hali halisi na kusikiza sauti halisi ya Harmonize.

Wadau mbali mbali katika tasnia ya muziki wamejitokeza na kumsifia Harmonize kwa talanta aliyonayo na pia kwa kuwakumbusha watu kuwa sanaa ni njia bora ya kupasha ujumbe.

 

Leave your comment