Harmonize Aomba Msamaha Kupitia Wimbo Mpya 'Sorry' [Video]

[Picha: Music In Africa]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mkurugenzi mtendaji wa Konde Music Worldwide Rajab Kahali almaarufu kama Harmonize kwa hali isiyotarajiwa amekosha mashabiki zake kwa kuchapisha video kwenye ukurasa wake wa  Instagram akitumbuiza wimbo unaoitwa "Sorry" 

Harmonize ambaye wiki chache zilizopita alitamba na "Sandakalawe" alichapisha video ya wimbo huo ikimuonesha yupo ufukweni juu ya jukwaa lililonakshiwa na maua mazuri huku yeye akitumbuiza kwa hisia wimbo uliojulikana kama "Sorry" huku bendi ya muziki ikiwa pembeni. 

Soma pia: Nyimbo Mpya: Alikiba, Mayorkun Waachia Wimbo Mpya 'Jealous'

"Sorry" ni wimbo wa mapenzi ambapo Harmonize anakiri makosa aliyoyatenda na anamuomba mpenzi wake amrudie kwani anateseka na kuumia sana ambapo watu wengi mtandaoni wametafsiri wimbo huo kama kitendo cha Harmonize kumuomba msamaha mke wake Sarah ambaye waliachana miezi kadhaa nyuma. 

"Mimi ni mwanadamu sijakamilika hadi siku ya mwisho watakaponizika usisahau Zuu hana kosa Malaika, fanya unisamehe" anaimba Harmonize kwenye aya ya kwanza. 

Harmonize anaendelea kumbembeleza mpenzi wake kwa kuonesha ni kwa namna gani anavyomuhitaji, anaimba "Namaliza wiki nyumbani sifiki, simu zako sishiki, mi sina marafiki ulinivumilia vingi na vyenye thamani kushinda shilingi" 

Kufikia sasa kwenye ukurasa wa Instagram wa Harmonize video hiyo ishatazamwa takriban mara laki 6 huku maoni yakiwa zaidi ya elfu kumi na katika hali isiyotarajiwa Harmonize hajachapisha video hiyo kwenye akaunti ya Youtube kama ambavyo ni kawaida kwa nyimbo zake nyingine. 

Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa msanii wa Kondegang kufanya video akitumbuiza wimbo, msanii Ibraah alitoa "Nitachelewa Acoustic" Oktoba 6 mwaka 2020 akitumbuiza wimbo wa "Nitachelewa"

Leave your comment