TANZANIA: Wimbo Mpya Wa ‘Happy’ Wa Rich Mavoko Waibua Mapya, Mashabiki Wake Wampongeza Kuondoka WCB

Tangu msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Rich Mavoko aachie ngoma yake mpya ya ‘Happy’ kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii maoni mengi ya mashabiki wake yamekuwa yakiongozeka kila siku wengi wakimpongeza.

Maoni hayo licha tu ya kumpongeza kwa kutoa ngoma kali bali pia yamekuwa yakimpongeza msanii huyo kuondoka kwenye lebo yake ya WCB.

Anyways tunaweza kusema maoni hayo ya mashabiki hayana uhalisia lakini je, kwa idadi ya watu hao wote ni kweli wanalolisema halina ukweli?

Na ni kwanini mashabiki wanamtangazia Rich Mavoko kuondoka WCB ile hali uongozi wa WCB na hata wasanii wenzake kutoka WCB wanakataa kuwa hajaondoka WCB?

Hii inatia hofu zaidi kwa Rich Mavoko kwani hata mfumo wa Q Boy msafi na Kifesi ulikuwa hivyo hivyo kuondoka WCB kila mtu alikataa kuwa hawana tofauti mpaka walipoamua wenyewe kufunguka.

Je, Rich Mavoko na wewe unasubiri hadi mashabiki wako wakushambulie mitandaoni ndio uje uongee? kwanini usiliweke wazi suala hilo kama ulivyoweka wazi wakati ule unasainiwa WCB.

Wahenga wanasema mficha maradhi kifo humuumbua, na ili uweze kuwa huru ni lazima uwaweke wazi mashabiki wako juu ya hatma yako ndani ya WCB hii itakufanya hata kama ni kweli umeondoka WCB uendelee kupendwa na mashabiki wako uliowavuna ukiwa WCB kwa miaka miwili.

Hebu fikiria shabiki wako wa WCB ambaye alizoea kuona kwenye BIO zako za mitandao ya kijamii umeweka lebo ya WCB lakini kwa sasa umefuta unadhani anapata picha nzuri kutoka kwako? bila shaka atakuchukia ni bora uwaweke wazi mashabiki wako.

Source: bongo5.com

Leave your comment