TANZANIA: Nafunga Ndoa Na Mtu Nimpendae - Billnass

Msanii wa muziki nchini Billnass, amedai kuwa anampango wa kufunga ndoa na mpenzi wake wa sasa itakapofika mwakani kwasababu anapenda maisha ya ndoa nakuwa na familia kwani ni kitu muhimu kwake.

Msanii huyo amesema hayo leo Juni 11, 2018 na kuongeza kuwa hatua ya kuingia katika ndoa inatokana na uamuzi wake mwenyewe na wala sio kusukumwa na watu au matukio aliyopitia katika maisha yake ikiwemo kufuta skendo ya video baina yake na msanii Nandy.

“Mimi nikiingia katika ndoa sio kwasababu ya kufuta skendo, naoa kwasababu naingia kwenye maisha ambayo nayapenda, familia kwangu ni kitu muhimu sana lakini pia naingia katika ndoa na mtu ambaye nampenda zaidi, ndoa ni mipango ya Mungu lakini kwa ratiba zangu nilikuwa natamani mwakani nioe” amesema Billnass.

Billnass aliongeza kuwa mpenzi wake wa sasa ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kumuunga mkono wakati wa kipindi kigumu alichopitia baada kusambaa kwa video yake na Nandy, amesema “Sijaachana na mpenzi wangu nipo nae mpaka sasa ni mtu mwenye akili na ndiyo mtu pekee niliyekuwa nawasiliana nae sana na kunifariji ni mtu anayejielewa”

Kwa upande mwingine msanii huyo amedai kwamba kusambaa kwa video yake na msanii wa kike Nandy lilikuwa ni jambo baya na alifanya makosa kwani lengo lake kama msanii, watu wamjue kupitia kazi zake na sio mambo ambayo yanaharibu taswira yake ya usanii.

Source: eatv.tv

Leave your comment

Other news