TANZANIA: Ngoma Tano Bongo Za Kimataifa Bila Video

Wasanii wa Bongo Flava wamekuwa wakionesha jitihada za kutaka kuufikisha muziki wao mbali. Si uishie Tanzania pekee bali hata katika nchi nyingine uweze kufika.

Kufanya kolabo na wasanii wa nchini nyingine imekuwa ikitumika kama njia rahisi zaidi ya kufanikisha hilo, wengi wamefanikiwa katika hilo. Hizi ni kolabo tano za kimataifa Bongo licha ya ukali wake hazikupata video.

Freeze – AY ft. P Square

Freeze ni miongoni mwa kolabo kubwa za kimataifa ambazo AY alianza kuzitoa, ni kipindi ambacho P Square wanaanza kuiteka Afrika na muziki wao.

AY ndiye msanii wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kufanya wimbo na kundi la P Square kutoka Nigeria, baada ya hapo wakafuata wengine kama Cindy Sanyu kutoka Uganda na Diamond Platnumz.

Wimbo Freeze ulitoka mwaka 2008, katika kipindi cha Mkasi AY alikiri kulifanyika makosa ya kutoa wimbo huo bila video kufanyika, ila amekuwa akihakikisha kosa hilo halijirudii tena katika muziki wake.

Tupogo – Ommy Dimpoz ft. J Martin

Ommy Dimpoz ni miongoni mwa wasanii wa Bongo walioweza kufanya kolabo na J Martin kipindi anasumbua vilivyo Afrika.

Baada ya Ommy Dimpoz kumshirikisha J Martin katika wimbo wake ‘Tupogo’ na kushindwa kutoa video ya wimbo huo, alikuja kutoa remix ya wimbo ambao alifanya pekee yake.

Hata hivyo Ommy Dimpoz si msanii pekee wa Tanzania kufanya kolabo na J Martin, kuna Mwana FA na AY ambao walimshirikisha katika wimbo wao uitwao Cheza Bila Kukunja Goti.

Mimi ni Mimi – Lady Jaydee ft. Oliver Mtukudzi

Kwa wanaoelewa maana ya muziki bila shaka kolabo hii wataiweka katika mizani ya juu kabisa kupata kutokea katika Bongo Flava.

Wakati Lady Jaydee akiongoza orodha ya wasanii wa kike Bongo wenye albamu nyingi akiwa albamu saba, Oliver Mtukudzi ni miongoni mwa wasanii wenye alamu nyingi zaidi Afrika akiwa na albamu zaidi ya 40.

Gwiji huyo muziki kutokea nchini Zimbabwe mwaka 2013 alishirikishwa na Lady Jaydee ambapo kwa pamoja walitoa wimbo uitwao Mimi ni Mimi.

Nakutunza – Barbana ft. Jose Chameleon

Hakuna asiyejua uzito wa jina la Jose Chameleon kwa upande wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Tangu mwaka 2000 anatoa albamu na hadi sasa akiwa na albamu zaidi ya 10.

Mwaka 2015 Barnaba alimshirikisha Jose Chameleon katika wimbo wake ‘Nakutunza’. Wimbo ulirekodiwa studio kwa Barnaba ‘High Table Sound’ ambapo inaelezwa kuwa Jose Chameleon alitumia zaidi ya saa 16 studio hapo kuhakikisha ngoma hiyo inafanikiwa.

Kutofanyika kwa video ya wimbo huu kuliibua uvumii kuwa Barnaba na Jose Chameleon hawaelewani, hata hivyo kupitia kipindi cha The Playlist, Times FM mwaka 2016 Barnaba alikanusha na kueleza video ya wimbo huu itatoka ila wimbo utakuwa katika version tofauti na ile ya awali.

Chacun Pour Soi – Papa Wemba ft. Diamond Platnumz

Wimbo huu ambao Papa Wemba alimshirikisha Diamond Platnumz ulitoka June 24, 2017 ikiwa ni miezi miwili imepita tangu kifo cha Papa Wemba aliyefariki April 24, 2017.

Wawili hao walikutana nchini Ufarasa ndipo wakarekodi wimbo huo hata hivyo kifo cha gwiji huyo wa muziki wa souks kutoka Congo kilipelekea kutofanyika kwa video ya wimbo huo.

Kutokana na hilo June 27, 2017 Diamond Platnumz alitoa documentary kuhusu na wimbo huo ikionyesha namna walivyourekodi wakiwa nchini Ufaransa.

Source: bongo5.com

Leave your comment

Other news