Lyrics
“JASIRI JOHN….. ALIYAANGALIA MAISHA YAKE,
HAKUONA JINSI ANGEWEZA KUISHI BILA JANE,
MSICHANA ANAYEMPENDA.
LICHA YA KUZONGWA NA UMASIKINI,
ALIJITAHIDI KUMPA JANE MAHITAJI MADOGOMADOGO KADRI ALIVYOWEZA,
View more
LAKINI ALIFAHAMU SHUBIRI YA KUSUBIRI KUPENDWA HUKU ANAFAHAMU KUSUBIRI KUPENDWA NI MATUMAINI YANAYOUMIZA. KAMA WANAVYOSEMA, MTAFUTAJI HACHOKI AKICHOKA KASHAPATA….ALIENDELEA KUNGOJA”
Ah! Sikuwa na zali sikuziamini ndumba,
Sikuwa na mali za kufuja,
Nilijitahidi kuuza mitumba kufuga mipunga,
Ili siku nimpe gari nimpe nyumba. Nilishindwa…
Niliishia kumpa chai, ‘chipsi’ mayai na ‘vocha’,
nywele za kimasai na mkoba,
Pesa za magauni, majuba na viatu vya kuzuga,
Nilimpa muda ila bado haikutosha, kwani…
Nilipomwambia nampenda hakujibu,
Akaweka moyo wangu maumivu,
Na mtima wangu akauweka ‘solemba’,
Nikaapia kuwa sitakuja kupenda ‘forever’,
Ah! Nilimpa upendo nilimpa sifa,
Niliweka mitego ya faida, haikuwa shwari,
Nikabadili mwenendo wa maisha,
Niliweka malengo sikutimiza, hakunikubali.
Alikuwa na ndoto kubwa kushinda mimi,
Alikuwa na misimamo kuipita dini,
Aliniambia ameomba nije kuokota utajiri,
Amengoja sana na sasa amechoka kusubiri,
“JOHN ALIFAHAMU HALI YA JANE, KUWA JANE ALIZALIWA KWENYE
FAMILIA MASIKINI, NA ALIUCHUKIA MNO UMASIKINI. ALIFAHAMU UMASIKINI ULIVYOCHUKUA UHAI WA MAMA YAKE KIPENZI, ALIYEFARIKI KWA KUKOSA MATIBABU. ALIIFAHAMAU NADHIRI ALIYOIWEKA JANE YA KWAMBA HATOKUBALI TENA KUISHI KWENYE MAISHA YA KIMASIKINI, NADHIRI ILIYO MWEKA JOHN NJIAPANDA”
Ah! Sikuwa na hali ya kuikosha roho yake,
Nilimwacha aende aufate moyo wake,
Alipata bwana wa kizungu magharibi
alimwahidi kuishi maisha ya ndoto zake,
Nilipata uchungu niliishia kuhamaki nilitaka nijiue,
Nilitaka nimzuie abaki nikakumbuka
ukipenda ua haulikati unaliacha likue.
Duka langu nilifunga biashara niliacha zote,
Uchumi uliyumba kwa maana nilianza pombe,
Niliumwa bado kidogo moyo uzime,
Nilimfanya ndoto kumbe naye ana ndoto nyingine.
Alisema anakwenda jiji la Miami,
Hakuna alichowaza zaidi ya kuishi kifahari,
Kamtumia picha na ‘mchizi’ kazikubali,
Na yupo tayari kumlipia gharama za safari.
Aliondoka na kipande kimoja cha mwili,
Nilikonda nilipata ugonjwa wa akili,
Haikuwahi kupita hata sekunde nisilie,
Nilitamani mpaka ardhi ipasuke niingie,
“JANE ALIPOONDOKA ALIMWACHIA JOHN KIDONDA KILICHOCHELEWA SANA KUPONA
NA YEYE AKAWEKA NADHIRI YA KUTOJIHUSISHA NA MAPENZI TENA MAISHANI MWAKE. ALIKAA KWA MUDA MREFU BILA MAHUSIANO. LAKINI…
HAKUNA DAKTARI MZURI KAMA MUDA, JOHN ALIPONA MAUMIVU NA ALIIRUDIA HALI YAKE YA KAWAIDA”
Ah! Muda ukaenda nitapata ‘Mwanamwali’,
Nikamwomba awe mwenza wa maisha akakubali,
Nikamvisha pete nikalipia mahari,
Sikumpenda lakini nilijifunza kumjali,
Aliuliza kama nampenda, nilimjibu,
Sikutaka kuweka moyo wake maumivu,
Sikutaka kuuweka Mtima wake solemba,
Kiasi aseme hatakuja kupenda ‘‘forever’’,
Ah alinikumbatia nikamfunga kwa ishara,
Akanikabidhi tunda nikala,
akaniamini tukajuana nikapanga kumwoa,
Akaidhisha na tukaanza na mipango ya ndoa,
“WAKATI KARNE YA 21 INAINGIA, JOHN ALIKUWA NI MIONGONI MWA
VIJANA WALIOKUWA ‘FASCINATED’ NA UKUAJI WA TEKNOLOJIA YA MITANDAO YA KIJAMII. ALIJIUNGA NA DUNIA HII MPYA, MARA KADHAA ALIKAA KWENYE UBARAZA, AKIANGAZA SIMU YAKE. AKIPAPASA KILA KITUFE, NDIPO SIKU MOJA AKAPATA UJUMBE KUTOKA KWA JANE”
“Habari naamini u bukheri wa afya,
Unaendeleaje maisha na huyo mpenzi wa sasa,
.nashukuru nahema ughaibuni si kwema
nakiona cha mtema mpaka naona ni heri nikafa…
Ah! Maisha niliyowaza yote ni uongo,
nauzishwa madawa nalazimishwa ngono,
nafungiwa ndani kama mtumwa ufungwani
Roho yangu rehani kiasi sasa naitamani Bongo,
Ukubwa umekuja kunisafisha jicho,
Ndoto imeisha na taswira imenionyesha sivyo, ah
naomba unifate uniondoshe kwenye hichi kifo,
na hii namba ya msamaria atakueleza nilipo”,
Sherehe ilikuwa na mipango madhubuti,
kabla mimi kuichukua michango ya Harusi,
Nikatoroka ughaibuni kufuata hisia zangu,
kwenda kumfata njiwa wangu mahususi,
Nilivuka majangwa na majabali,
Sehemu ya safari anga sehemu nyingine bahari,
Niliacha kila kitu nyuma upendo na huruma vilinijaa,
penzi likanipeleka mbali,
“JOHN ALIFIKA UGHAIBUNI, AKAMTAFUTA MSAMARIA ALIYETAMBULISHWA NA UJUMBE, MSAMARIA AKAMWELEKEZA NJIWA WAKE ALIPO, NA NIKWELI… HAPAKUWA PEMA”
nikakutana na bopa la kizungu,
Lenye sura ya kuichachisha mboga kwenye chungu,
Kiko kwenye mdomo,Tatuu kila kona na wapambe
pamoja na vishoka wenye mtutu.
Sio siri alizungukwa na wasichana wengi,
Sikujua umri walikuwa wadogo ka’ “madent”,
Baadhi walikuwa uchi wanahesabia “chenchi”,
Wengine masaji huku wengine wanamchezea nyeti.
“MASIKINI JOHN, ALIDANGANYA KWA KUJITAMBULISHA KAMA KAKA KWA JANE, AKIMSIHI YULE MAFIA AMRUHUSU AONDOKE NA JANE WAKAANZE MAISHA MAPYA, LAKINI… PALIPOSHINDWA SHOKA WEMBE HAUWEZI TAMBA. KWA KUZIDIWA NA UOGA WA KUUAWA…JANE ALIMKANA JOHN KWA KUSEMA HAMJUI…”
Hata nilipomuuliza kama ananipenda hakujibu,
Akaweka moyo wangu maumivu,
Nilijua hawezi kufa kwa sababu hakunipenda
Na ni rasmi nikapoteza shilingi kwenye msitu,
Nilikiambia kifo kama unakuja njoo,
Maana sikuwa mtu ilishakufa roho,
Sikuumia kama alivyoniumiza yeye,
Kwahiyo sikujali jinsi nilivyoteswa na wale mbwa no,
Aliambiwa ambusu bosi hakubisha,
Alipewa bunduki hakusita,
Aliishika risasi akaiingiza
Akaambiwa anipige kwenye kichwa,
JOHN ALIKUWA NI JINA JIPYA LA WAHANGA WA UPENDO WA DHATI, VIPOFU WA MAPENZI, WAJINGA WA MAHABA...
JOHN ALIKUWA ROMEO KWENYE ROMEO AND JULIETH, ALIKUWA SAMSON KWA DELILAH KWENYE WAHUKUMU WA AGANO LA KALE, ALIKUWA JACK KWENYE TITANIC, FRED WEASLEY KWENYE HARRY POTTER..
JOHN ALITUKUMBUSHA KUWA UPENDO NI SADAKA, SADAKA YA MUDA NA PESA, ALITUKUMBUSHA UPENDO NI SADAKA YA DAMU.
JOHN, ALIPOTEZA UHAI AKIWA KWENYE SAFARI YA KUTAFUTA UPENDO WA MTU ALIYEMHUSUDU NA
JANE ALIPOTEZA AMANI NA THAMANI YAKE KAMA MTU AKIWA KWENYE SAFARI YA KUTAFUTA UTAJIRI ALIOUHUSUDU
Hatia iko wapi?