TANZANIA: Snura aomba radhi na kukabidhiwa usajili mpya na BASATA

Snura amewaomba radhi watanzania kwa video ya wimbo wake ‘Chura’ inayowadhalilisha wanawake na iliyo kinyume na maadili.

Muimbaji huyo amekutana na waandishi wa habari Alhamis hii kwenye ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.

“Aidha tunaomba radhi vyombo vya serikali, vinavyosimamia sekta ya sanaa kwa kutokufuata sheria, kanuni na taratibu katika uendeshaji wa shughuli za sanaa hapa nchini. Mimi kama meneja na msanii wangu tunaahidi hatutarudia tena kufanya tukio hilo la udhalilishaji, na iwapo tutarudia adhabu kali juu yetu zichukuliwe,” aliahidi HK ambaye ni meneja wa Snura.

Aliongeza, “Pia naahidi kuwa mfano bora kwa jamii inayotuzunguka, wasanii wenzetu katika kutunza na kufuata maadili na tamaduni zetu pamoja na sheria za nchi. Hii ni pamoja na kufuata sheria katika mamlaka na taasisi, tunafamu kwamba baadhi ya wasanii hasa hasa wa kizazi kipya, hawajajisajili Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama ilivyokuwa kwa msanii wangu, Snura. Lakini kwa sasa baada ya kupata maelekezo kutoka BASATA, Snura ameshajisajili. Pia tunawashauri wasanii kabla ya kufanya video ya wimbo, waende Bodi ya Filamu kwa ajili ya kupata vibali. Mwisho kabisa tunaahidi kutekeleza maazimio na maelekezo yote yaliyotolewa katika kikao cha Wizara. Maagizo hayo ni kutoa video kwenye mtandao wa YouTube na hilo tumeshalitekeleza, kujisajiri BASATA , tayari tumeshajisajili, na tatu ni la kuifanya upya video ya Chura ambapo mpaka sasa tumeshaandaa script na ipo Bodi ya Filamu inakaguliwa na kila kitu kinaenda sawa.”

Jana video na wimbo huo vilifungiwa na wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo kwa madai kuwa inakiuka maadili ya Kitanzania. Pia alizuiwa kufanya maenesho ya hadhara kwakuwa hajajisajili kwenye baraza la sanaa la taifa, BASATA.

 

 

Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, Snura amedai kuwa tayari amekamilisha mchakato wa usajili na BASATA imempa kibali. Pia amedai kuwa amewasilisha video mpya ya wimbo huo kwa bodi ya filamu ya Tanzania ambayo itaikagua.

 

 

 

Leave your comment