TANZANIA: Producer analipwa laki 2, lakini director analipwa milioni 30…! Inasikitisha – Mater J

 

Producer mkongwe nchini wa muziki ambaye pia anamiliki studio ya MJ Productions, Master J, ameleeza kusikitishwa kwake na hali ya kudharaulika kwa maproducer wa audio music ikilinganishwa na madirector wa video.

Master J amesema hayo alipokuwa katika kipindi cha Friday Night Live (FNL) kinachorushwa na EATV kila Ijumaa saa 3:00 hadi saa 5:00 usiku.

Mkongwe huyo alikuwa akijibu swali la mtangazaji Sam Misago lililotaka kujua ni kitu gani ambacho producer huyo anakichukia zaidi katika muziki wa bongo flava.

Master J alisema kuwa kitu asichokipenda zaidi katika bongo flava ni kuona msanii anakuwa tayari kumlipa director wa video mamilioni ya shilingi huku producer wa audio ya ngoma hiyo hiyo akimlipa kiduchu.

“Maproducer Tanzania wanadharaulika sana, wasanii wanasahau kuwa bila beat huwezi fanya chochote, wimbo wako hauwezi kupigwa kokote, haupigwi kwenye redio wala TV, sasa sielewi hii dharau ni ya nini, yaani producer analipwa laki 2, lakini director analipwa milioni 30…! Inasikitisha” Alisema Master J.

Amekiri kuwa hiyo ni sababu moja wapo inayosababisha maproducer wengi hivi sasa kukimbilia kufanya kazi za matangazo badala ya muziki kwa kuwa hawaoni wakipewa thamani wanayostahili.

“Kuna wakati nilimwambia Daxo, kama msanii hataki kukulipa vizuri muache akafanye show kokote hata kama ni Biharamulo huko bila beat, aende na video yake kama wanadhani video ni muhimu kuliko audio” Alisisitiza Master J.

Kwa upande wake msanii Mkongwe wa hip hop nchini Mr. Two a.k.a Sugu ambaye aliongozana na Master J katika kipindi hicho kwa lengo la kuzindua rasmi video mpya ya Sugu ya ngoma ya Freedom, alimshauri Master J kuungana na maproducer wengine kuanza harakati za kudai heshima wanayostahili.

 

 

 

Leave your comment