TANZANIA: Daxo Chali athibitisha rasmi kuwa ngoma ya ‘Freedom’ ni ya Sugu.
2 May 2016
Utata uliokuwa umeghubika umiliki wa ngoma mpya ya Mr Two a.k.a Sugu inayokwenda kwa jina la Freedom umemalizwa katika show ya FNL baada ya producer wa ngoma hiyo Daxo Chali kuthibitisha rasmi kuwa ni ngoma halali ya Sugu.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa msanii Mr Blue aliyekuwa akidai kuwa Sugu amebadilisha ngoma yake aliyokuwa amemshirikisha, na kuondoa mashairi yake bila ya ruhusa yake, na kasha kuitoa kwenye media.
Akiwa katika kipindi cha FNL kinachoruka kupitia EATV usiku wa Ijumaa, producer wa ngoma hiyo kutoka MJ Records Daxo ambaye pia ndiye aliyekuwa ametengeneza ngoma ya Mr Blue na Sugu, alisema kuwa alichokifanya ni kuchukua ‘beat’ ileile na kumpa Sugu kwa ajili ya ngoma nyingine.
Daxo amesema alifanya uamuzi huo kwa kuwa ‘beat’ ile ni mali yake, na pia aliona kuwa ngoma aliyokuwa amefanya Mr. Blue haikuwa “serious” hivyo baada ya kupata wazo la kutoa ngoma ambayo ni serious kutoka kwa Sugu akaamua kufanya hivyo.
Akiwa ameongozana na Sugu mwenyewe pamoja na mmiliki wa studio za MJ Record, Master J, Daxo amesema kuwa alichokifanya ni halali kwa kuwa katika muziki, ‘beat’ ni mali ya producer.
“Mwanzo kabisa Blue aliongea na Marco Chali, baadaye mimi nikamsikilizisha hii beat ikiwa pamoja na chorus yake, hiyo chorus nimefanya mimi, Blue akaipenda, akaja kufanya ngoma na Sugu lakini ngoma ile haikutoka official, baadaye Sugu akaja, tukampa, kile ambacho ni mali yetu, mashairi ya blue tukayatoa kwa kuwa ni mali yake” Alisema Daxo
Katika kipindi hicho kilichoanza saa 3:00 hadi saa 5:00 usiku, Daxo aliongozana na Sugu pamoja na Master J ambao wote walionesha kushangazwa na kitendo cha wasanii wa kitanzania kutoelewa masuala ya haki miliki za muziki na kwamba ‘beat’ yoyote inayotengenezwa na producer ni mali ya producer na ndiye mwenye haki zote.
“Kibongobongo msanii akishakulipa pesa ya kumtengenezea ngoma, basi anaona yeye ndiyo kila kitu, anaona anaweza kuifanyia chochote ile beat ambayo producer umemtengenezea, kitu ambacho siyo sahihi, siku zote ‘beat’ ni mali ya producer” Alisema Master J.
“Sina cha kusema na ningependa huo mjadala sasa ufungwe na tutumie fursa hii kujifunza masuala ya copy rights, tatizo wasanii wengi wakiitwa kwenye semina za masuala kama haya hawatokei” Alimalizia Sugu
Unaweza kuitazama video ya wimbo wa Freedom hapa:
Leave your comment