TANZANIA: BASATA yawatahadharisha wasanii dhidi ya matapeli

 

 

Baraza la Sanaa la Taifa lawataka wasanii kuwa makini dhidi ya mapromota au baadhi ya wanaojiita wadau wa Sanaa ambao wamekuwa wakitumia njia za kilaghai na utapeli katika kujipatia faida na manufaa kupitia mgongo wa wasanii.

Baraza limetoa angalizo hilo baada ya kuwepo kwa ongezeko la matukio ya baadhi ya watu wanaojiita wadau wa Sanaa ambao wamekuwa wakiwadanganya wasanii kwa kuwaahidi fursa mbalimbali kama za maonesho ya ndani na nje ya nchi. Ambapo hata hivyo zimekuwa zikiishia katika kuwaletea wasanii matatizo ya kiuchumi.

Pia watu hao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi wa Serikali kuwatapeli wasanii na kujipatia fedha isivyo kihalali.

BASATA linapenda kuwakumbusha wasanii kwamba kabla hawajaingia kwenye makubaliano yeyote na mtu, asasi au kampuni yoyote wawasiliane na mwanasheria au watoe taarifa Ofisi za Utamaduni za wilaya au manispaa zilizo karibu ili kuhakikisha wanaepuka ulaghai na udanganyifu toka kwa watu hao wasio waaminifu.

Aidha, kwa wasanii walioko Dar es salaam BASATA linawaelekeza kufika ofisi zake zilizoko Ilala Shariff Shamba, ili wapate msaada wa kisheria na kujiridhisha kama makubaliano yao ni halali nay a uhakika.

Mwisho kabisa BASATA linapenda kuwakumbusha wasanii kwa ujumla kwamba, tangu januari mosi 2013 tasnia ya muziki na filamu ni rasmi hivyo wasanii wote hawana budi kusajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, Kanuni na utaratibu za uendeshaji wa kazi za Sanaa nchini.

Pia ni wajibu, kwa kila msanii kuhakikisha anafanya kazi na mtu, watu, asani au kampuni iliyo na vibali halali vya kuendesha shughuli za Sanaa na si vinginevyo.

Sanaa ni Kazi Tuituze, Kuikuza na Kuithamini.

Godfrey Mngereza

Katibu Mtendaji - BASATA

 

Leave your comment