TANZANIA: Chege aeleza kwanini yeye na Temba wanasikiaka zaidi Wanaume Family!

Rapper Chege kutoka kundi la TMK Wanaume family, amesema kundi lao lina wasanii zaidi ya 7 ila kwa sasa mfumo wa biashara ya muziki umebadilika ndio maana mara nyingi hawatoi kazi ya kundi zima.

Msanii huyo anayefanya vizuri na wimbo wake wa ‘Sweety Sweety’ amekiambia kipindi cha Uhondo cha E Fm kuwa, yeye na Temba tayari wametengeneza ‘Chemistry’ ambayo mara kwa mara mashabiki wamekuwa wakiihitaji.

“Wakati ule tunafanya kazi za kundi watu 7 au 8, muziki ulikuja ukachange, mashabiki wakawa wanahitaji sauti ya Chege na Temba peke yake”, alisema Chege.

“Tukajaribu kufanya ngoma moja inaitwa ‘Twenzetu’, tulifanya mimi, Temba na marehemu ‘YP’ pamoja na Ferouz ikapendwa sana, ndio ngoma ambayo ilinitambulisha mimi. Baada ya kutoa hiyo ngoma mimi nikatoa albamu yangu ambayo ndani yake kulikuwa na hiyo ngoma, wakati huo tulikuwa tunauza albamu kwa muhindi ‘Mamu’. Mamu akamwambia Fella mimi namtaka Chege na Temba, sisi tukaingia studio tukafanya albamu ya ‘Mkono mmoja’ ikafanya vizuri sana”.

Pia Chege aliongeza kutokana na hiyo albamu mashabikia wakajua wametoka Wanaume Family lakini haikuwa hivyo. Mbali na hivyo pia alidai kuwa kundi la Wanaume Family bado lipo na lina wasanii 7 ila kwa sasa wanaangalia upepo unavyokwenda na ndio maana wanasikia zaidi yeye na Temba.

Wawili hao wameachia singo mpya, Chege anatamba na video ya ‘Sweety Sweety’ na Temba katoa wimbo uitwao ‘Fundi’.

Leave your comment