EXCLUSIVE (TANZANIA) – Wasanii wachanga watakavyonufaika na Sheria ya TV na Radio kuwalipa wasanii – Waziri Nape Nnauye
18 December 2015

Maswali mengi yameibuka tangu itangazwe sheria ya wanamuziki wa Tanzania kulipwa na vituo vya Radio na Televisheni kwa kutumia kazi zao. Moja ya maswali hayo ni kuhusu kama sheria hii itakuwa na manufaa kwa wasanii wachanga au itachangia kuwapa wakati mgumu zaidi ya kupata nafasi ya kazi zao kuchezwa.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amefafanua jinsi wasanii chipukizi watakavyonufaika na utaratibu huo unaotarajiwa kuanza kutumika Januari, 2016.
“Wapo watu wanasema sheria hii ya wanamuziki kulipwa inaweza kuwaumiza wanamuziki wachanga, lakini mimi nadhani si kweli kama ukifanya kazi nzuri hata kama umeingia leo sokoni kazi yako itahit tu, na bahati nzuri ni kwamba hata ukifanya kazi moja ikahit vizuri utapata kipato. Kwahiyo tutawasaidia hata wale wanamuziki wachanga, msaada watakaoupata ni kwamba kazi zao zikipigwa watalipwa kwasababu ukiwa mchanga sana mpaka ukaanze kupata kipato cha maana kwenye ulimwengu wa muziki kwa sasa ni shughuli kubwa, lakini kama sheria hii ipo manaake hata kama wewe ni msanii mchanga kama ukaingia na single yako ambayo ikapiga vizuri unaweza ukajikuta umepata mtaji wa kutengeneza album na wa kufanya mambo mengine makubwa zaidi”, Alisema Waziri Nnauye kupitia XXL ya Clouds FM.
Katika suala zima la jinsi gani vituo vitakuwa vikiwalipa wasanii, Nape ameeleza;
“Kimsingi formula iliyopo ni kwamba tunachukua asilimia ya mapato uliyoyapata kutokana na matangazo, ile ndiyo itakayotolewa asilimia 30 kupata kiasi gani utawalipa Cosota kwa ajili ya kulipia muziki uliotumia. Kwasababu kila redio au kila TV pamoja na matangazo inapiga muziki na ule muziki kwa sehemu kubwa inachangia kuongeza idadi ya wasikilizaji katika ile Radio… Kwa vyovyote vile hakuna radio ambayo inajiendesha bila tangazo kabisa haipo, lazima kutakua na tangazo hata kama ni dogo .., na sisi tutachukua asilimia hicho hicho kidogo ambacho unacho, tuwape Cosota kwasababu kwa vyovyote vile utakuwa umepiga muziki wetu kwahiyo tuwape Cosota, Cosota wawafikishie walengwa”, Waziri Nape alimaliza kwa ufafanuzi huo.




Leave your comment