EXCLUSIVE (TANZANIA) – Hussein Machozi atangaza kuacha rasmi muziki baada ya single yake ya mwisho!

 

 

Msanii wa muziki wa Bongo Fleva Hussein Machozi ametangaza uamuzi wake wa kuacha kufanya muziki, kutokana na kutopata faida yoyote anayoipata kupitia muziki kwa muda mrefu.

Machozi ambaye ni msanii wa muda mrefu katika muziki wa Bongo Fleva, ambaye jina lake halisi ni Husseini Rashidi ambaye amewahi kuhit na nyimbo kama ‘Utaipenda’, ‘Kwaajili yako’, ‘Promise’ na nyinginezo.

Hussein ametangaza uamuzi huo kupitia Planet Bongo ya East Africa Radio,

“ Kubwa ambalo nataka niwasimulie Watanzania ambalo ninalo leo hii kwamba very soon ntaachia ngoma yangu mpya na ya mwisho kabisa kwa Hussein Machozi, namaanisha naacha muziki, naacha Bongo Fleva nakuwa mtu wa kawaida raia wa kawaida ambaye nitaishi maisha yangu ya kawaida” alisema Hussein Machozi.

Alitoa sababu ya kuchukua maamuzi hayo magumu kwake;

“Sababu ni kwamba kuna kitu kimoja ambacho kikubwa nakifanya kwenye maisha yangu ambacho kitanibadilisha maisha yangu kiurahisi kwasababu ninakimudu kufanya” alieleza.

“Nasikia vibaya sana na inaniuma sana kuwaacha Watanzania kwa style kama hii, ukiangalia kwa hali ya haraka haraka huwezi kuendelea kufanya kitu ambacho hakikuingizii kwasababu maisha yamebadilika, huwezi kuwa unafanya muziki tu unatoa muziki wenyewe hauingizi” alisema Machozi.

Pia msanii huyo aliongeza kuwa anatarajia kutoa wimbo wake mpya wiki mbili zijazo ambao ni zawadi kwa mashabiki waliomsupport kwa kipindi chote alichokuwa akiwaburudisha.

“ Na pia nafanya hivyo kwasababu ya heshima ya Watanzania sipendi kuwaacha vibaya kwahiyo nimeamua kuwapa zawadi ambayo itatoka baada ya wiki mbili kwa heshima kwasababu bado nina mapenzi kwao siwezi tu kuondoka hivi hivi ni bora niwaache na kitu ambacho angalau watakaa kukumbuka Hussein Machozi alituachia kitu hiki wakati anaacha muziki” alimaliza Hussein Machozi.

Leave your comment

Top stories