Mbosso: Safari Ya ‘Superstar’ Wa Bongofleva
18 February 2025
[Image Source: Instagram]
Writer: Elizabeth Betha
Download Kamba Dj Mixes On Mdundo
Mbwana Yusuph Kilungi almaarufu kama Mbosso ni msanii wa muziki wa kizazi kipya yaani Bongofleva ambaye ukiachana na kipaji chake ni mkali wa uandishi wa mistari inayofikirisha na kufurahisha, kuwafanya mashabiki zake na wapenda muziki mzuri kuimba sana nyimbo zake.
Kwa mara ya kwanza tulitambulishwa Mbosso kupitia kundi la muziki lililojulikana kama Yamoto Band mnamo mwaka 2013 ambapo alikuwa na wenzie watatu Aslay, Beka Flavour, Enock Bella na yeye mwenyewe Mbosso, bendi hiyo ilikuwa chini ya moja ya waasisi wa makundi maarufu ya Bongofleva Mkubwa Fella. Hapo waliweza kutoa ‘hits’ za kutosha kama Nitakupwelepweta, Niseme, Nitajuta, Nisambazie Raha, Mama na nyingine kibao. Japokuwa alikuwa kwenye kikundi na wenzie wenye vipaji lakini bado aliweza kung’ara kwa nafasi yake. Mwaka 2015 Yamoto Band walinyakua tuzo ya Bendi Bora kwenye tuzo za Muziki za Kilimanjaro (Kilimanjaro Music Awards), lakini mwaka huo huo kundi lao lilifika ukomo kwa kila mmoja wao kutaka kufanya kazi binafsi.
Mwaka 2018 Mbosso alirejea tena kwenye tasnia baada ya kusainiwa chini ya ‘label’ ya muziki inayokulikana kama WCB Wasafi iliyo chini ya Diamond Platnumz, na kuanzia hapo safari yake ya mafanikio kimuziki ilianza kwa ukubwa. Aliweza kuachia ‘hits’ za kutosha ikiwemo Hodari ambayo ilimfanya kupata tuzo ya Video Bora ya Mwaka kwa Tanzania kwenye HiPipo Awards mwaka 2019, lakini pia ‘hits’ zingine zilizompa tuzo ni Nadekezwa na Tamu ambazo alipata kutoka tovuti ya muziki Boomplay kwa kuwa nyimbo zilizopata wasikilizaji laki tano kwa muda mfupi toka ziachiwe, hivyo kumfanya Mbosso kuwa moja ya wasanii wanaofuatiliwa sana.
Muziki wake ni muunganiko wa ladha za kisasa na muziki wa asili ya nyumbani (Tanzania) na hiyo imeufanya muziki wake kuwa wa kipekee unaokonga nyoyo za mashabiki wa ndani na nje ya Tanzania, husasani nchi za Kiarabu ambako amekuwa akifanya matamasha mara kwa mara. Mashairi yake yamejaa hadithi za mahusiano, mapenzi na matukio ya kijamii ambayo kwa ukubwa wake yanagusa maisha ya mtu yoyote hivyo kumfanya kusikilizwa na watu wengi.
Mwaka 2021 aliachia albamu yake ya kwanza aliyoipa jina Definition of Love iliyokuwa na nyimbo 12 iliyokuwa na nyimbo 12 zikiwemo Mtaalamu, Baikoko, Kamseleleko, Tulizana aliyowashirikisha wana- Njenje (Kilimanjaro Band), albamu ilifanya vizuri na ni kati ya kazi nzuri kutoka kwake. Mwaka 2022 aliachia EP yake aliyoipa jina Khan, ina nyimbo 6 ambazo ni Huyu Hapa, Yataniua, Shetani, Pole, Assalaam na Wayo humo ndani alishirikisha wasanii wa ndani nan je ya Tanzania ikwemo Diamond Platnumz, Ruby, Ya Levis (France), Costa Titch (South Africa) Mohammed Almanji (Oman).
Mwaka 2025 ameuanza kwa kutoa hit nyingine aliyoipa jina ‘Kupenda’, amabapo kama ilivyo kawaida yake ni kazi nzuri iliyojaa ufundi wa Mbosso Khan mwenyewe. Hivi karibuni ziliibuka tetesi za yeye kuondoka chini ya label ya WCB Wasafi, na kiongozi wa label hiyo Diamond Platnumz amethibitisha hilo na kumtakia heri zote. Kuondoka kwake kunaweka alama ya kufungua ukurasa mpya katika safari yake ya muziki na sote tuko na ari ya kuona makali yake kama msanii anayejitegemea, na ni wazi hatatuangusha kwasababu yeye ni Mbosso.
Leave your comment