Umuhimu Wa Kollabo Na Remixes Kwenye Bongofleva

[Image Source: Instagram]


Writer: Elizabeth Betha
Download Kamba Dj Mixes On Mdundo

Wasanii wa Bongofleva wamekuwa wakifanya muziki wa aina tofauti na katika kuwakilisha kazi zao katika jamii, wameweza kutumia aidha ‘beats’ tofauti au pia kushirikisha wasanii wenzao ili kuleta ladha tofauti kwenye wimbo mmoja ambao ushatoka au unaotoka tayari ukiwa na wasanii zaidi ya mmoja.

Ufanywaji wa kollabo umezaa nyimbo nyingi ambazo zinaishi hadi leo kama Mashallah yake Chid Benz akiwa na Mzee Yusuf, Kama Zamani yake Mwana FA akiwa na Kilimanjaro band na Mandojo na Domokaya, na nyingine nyingi.

Lakini pia kuna ‘remixes’ nyingi zilizofanywa na wasanii wa Bongofleva ili kubadilisha na kuleta ladha tofauti katika nyimbo zao walizotoa zikiwa na aidha ‘beat’ tofauti au mashairi na wasanii tofauti. Kiujumla katika tasnia ya muziki, kufanya kollabo au ‘remix’ ni namna nzuri ya kuonesha ubunifu lakini pia kugusa mashabiki kwa namna ya kipekee.

Tukiangalia kwa mwaka ulioisha wa 2024, kulikuwako ‘remixes’ na kollabo za kutosha ambazo zimefanya vizuri na huenda bado zinaendelea kufanya vizuri hadi sasa ikiwa tayari tuko siku kadhaa ndani ya mwaka mpya. Ningependa kuzungumzia chache tu ili kuonesha kinachozungumziwa kuwa ni cha kweli.

Nandy alitoa wimbo wake wa Dah! akiwa na Ali Kiba, lakini baada wimbo kupokelewa vizuri na mashabiki na kufanyiwa ‘challenges’ za kutosha ‘TikTok’ na kwingineko alitoa ‘remix’ yake akiwa ameshirikisha wasanii wa Bongo Hip Hop na wa Bongofleva, kati ya hao walikuwepo Rosa Ree, Young Lunya, G-Nako nk. Remix hiyo ilifanya vizuri sana na kusaidia kuipeleka mjini zaidi ngoma hiyo na kupokelewa na si tu mashabiki wa Nandy, bali pia wasanii wengine aliowashirikisha.

Vanillah Music aliachia ‘hit’ yake ya Hakunaga akiwa na Ibraah kutoka Kondegang, kollabo yenyewe tu ilikuwa ni kali na ni wazi mashairi, ubunifu na wasanii wenyewe walisaidia kuipa ngoma nzima hadhi ya kuwa ‘hit’. Vanillah alidokeza uwepo wa ‘remix’ ya wimbo huo akitaka kushirikisha wasanii wengine, ikiwemo Tommy Flavour, ni wazi kwamba aliona umuhimu wa kuifanyia ‘remix’ ngoma yake.

Nyingine kali ilikuwa yake Chino Kidd, Bongoman kollabo ambayo tayari ilikuwa hatari, lakini karibia na mwisho wa mwaka, ‘remix’ yake ikatolewa akiwa  ameongezwa Mbosso Khan, na aliua sana na ni moja ya verse zilizopendwa sana na kuifanya ngoma iende mjini zaidi. Mashabiki wa Chino na Mbosso wote walifurahishwa na  bado wanaruka na Bongoman kitaani.

Aslam TZ aliachia ngoma yake ‘Tukutane Mwakani’ akiwa mwenyewe na ilifanya vizuri, lakini muda mfupi badae aliachia ‘remix’ ya wimbo huo akiwa na Masauti na Mabantu. Ni wazi ‘remix’ ilifanya na inaendelea kufanya vizuri hata sasa na imekuwa moja ya kazi nzuri kutoka kwa Aslam TZ kwa mwaka ulioisha.

Ukiachana na ubunifu na kuongeza ladha tofauti, kollabo na ‘remixes’ zinaunganisha mashabiki na kumfanya msanii ambaye alikuwa aidha hajulikani na mashabiki wa msanii mwingine kujulikana na zaidi kumuongezea mashabiki. Share hapo chini kwenye uwanja wa comments kollabo ama ‘remix’ yako bora ya miaka yote.

Leave your comment