Uchambuzi Wa Albamu Ya Therapy Ya Jay Melody

Image Source: Online 

Writer: Charles Maganga 

Baada ya kuidokeza kwa muda mrefu hatimaye Jay Melody ameachia albamu yake ya kuitwa "Therapy"

Therapy ni albamu ya kwanza kutoka kwa Jay Melody tangu aanze safari yake ya muziki mwaka 2017, ikiwa pia ni albamu yenye ngoma 14 ambapo 2 kati ya hizo ameshirikisha wasanii wengine. 

 

Kwa msanii kama Jay Melody ambaye anajulikana kwa ngoma zake kali za mapenzi, Therapy ni albamu ambayo imekuja kuendeleza na kukoleza safari ya Jay Melody kwenye muziki

 

Hizi hapa ni baadhi ya ngoma bora kutoka kwenye albamu hiyo iliyopokelewa vyema na mashabiki hadi sasa: 

 

1. Bado

Akiwa ameshirikisha wasanii kama Marisah, Karma, Ndelah na Benson kwenye ngoma hii Jay Melody anaimba kuhusu maisha na jinsi ambavyo anaendelea kupambana. Kwa msanii ambaye mara nyingi anaimba ngoma za mapenzi, Bado imekuwa ni kama surprise kwa mashabiki wengi. 

2. Forever 

Kwenye mkwaju huu, Jay Melody anatoa ahadi ya kutomuacha mpenzi wake daima. Jay Melody anatumia sauti yake tamu kufikisha ujumbe wake huo ambao bilashaks utakosha mashabiki wengi wa jinsia ya kike. 

 

3. Nahodha 

Kwa wapenzi wa muziki aina ya Baibuda basi ngoma hii ya kuitwa “Nahodha” ni maalum kwa ajili yao. Humu ndani Jay Melody anatumia lugha ya kisanii na tamathali za semi kuonesha jinsi mahusiano yake yanavyosambaratika na kuvunjika, akitumia utulivu mkubwa na ufundi wa lugha kufikisha ujumbe huo. 

 

4. Wa Peke Yangu 

Moja ya sifa kubwa ya Jay Melody kwenye kiwanda cha Bongo yni uwezo wake wa kutengeneza kiitikio au chorus yenye mvuto na ufundi huo ameuonesha kwenye “Wa Peke Yangu”. Kwenye mkwaju huu wa Bongo Fleva, Melody anasisitiza kuwa hachangii mapenzi na mtu na kwamba mpenzi wake ni wa kwake peke yake. 

 

5. Usiniache 

Ushirikiano baina ya Jay Melody na Phina ulianza kuonekana kwenye “Manu” na wawili hao waliamua kupeleka chemistry yao mbele zaidi kupitia ngoma hii ya “Usiniache” ambayo kimashahiri Jay Melody na Phina hawana mengi ya kusema zaidi ya kupeana ahadi ya kutokuachana. 

 

6. Watu 

Kuna namna ambayo Jay Melody ameweza kuichanganya vyema Bongo Fleva na muziki aina ya Kizomba kwenye ngoma hii ya “Watu”. Ndani ya ngoma hii Jay Melody anaonesha ni kwa namna gani ana ujasiri wa kumuonesha mpenzi wake mbele za watu. 

7. Unanimaliza 

Kwa jinsi mashahiri na miondoko ya ngoma hii ilivyo, ni dhahiri shahiri kuwa Jay Melody alikuwa ana lengo la kuitumia “Unanimaliza” ili kuuteka mtandao wa Tiktok. Beat tamu, mashahiri mepesi na ujumbe murua uliopo kwenye “Unanimaliza” ni ushahidi tosha kuwa Jay Melody ni mwalimu haswa wa kuandika ngoma za mapenzi

8. Diamond 

Ukweli ni kuwa ngoma hii haina uhusiano wowote na msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz badala yake Jay Melody anamuimbia mpenzi wake kwa kumsifia kuwa anang’aa kama madini aina ya Diamond yaani Almasi. 

9. 18

wa mtu yeyote ambaye alishawahi kuingia kwenye mahusiano bila kujua ameingiaje basi ngoma hii ni muhimu sana kuisikiliza kwani humu ndani Jay Melody anaonesha kushangazwa kwa namna ambavyo ameingia kwenye mahusiano na ampendaye “bila malengo” 

 

10. Sielewi

Kama uliipenda “Nakupenda” pamoja na “Nitasema” basi bila shaka utaipenda na ngoma hii ya kuitwa “Sielewi” yenye sauti tamu ya Jay Melody na ambayi itakosha mashabiki hasa wenye jinsia ya kike. 

 

11. Sio Sawa

Ukisikiliza ngoma hii kwa makini unaweza kudhani Jay Melody ana-rap lakini kumbe ni namna tu alivyochagua miondoko ya ngoma hii ya tofauti pamoja na stori ya ngoma hii kuwa ya kipekee tofauti na ngoma nyingine za kwenye albamu zilivyo. 

12. Siyawezi 

Kwenye ngoma hii, Jay Melody anaweka wazi kuwa hawezi kuendelea na mapenzi kutokana na tabia zisizofaa za mpenzi wake. Kwenye ngoma hii Jay Melody anatoa ujumbe wenye huzuni pamoja na kwamba mkwaju huu, kimashahiri sio wa kuhuzunisha sana. 

13. Katika 

 Kwenye albamu ambayo ina miondoko ya taratibu na ngoma zenye mahadhi ya kipwani, “Katika” inasimama kama ngoma ambayo ina utofauti sana na ngoms nyingine kwani beat ya ngoma hii ina mahadhi ya kuchezeka na vibe la kutosha, tofauti na ngoma nyingine kwenye albamu. 

 

14. Superstar

ay Melody anaimaliza albamu yake ya “Therapy” na ngoma ya “Superstar” ambayo ndani yake Jay Melody anaweka wazi kuwa yeye ni superstar na kwamba mashabiki wanamfahamu kama moja ya watu mashuhuri. 

 

Leave your comment