Biography: Msamiati, Rapa Anayepeperusha Vyema Bendera Ya Muziki Wa Hip Hop Tanzania

Image Source: Online

Kama unapenda muziki wa Hip Hop kutoka Tanzania basi bila shaka utakuwa unafahamu Msamiati, rapa ambaye kwa sasa anatamba na ngoma yake ya "Tumeondoka" ambayo amemshirikisha Joh Makini na Conboi.

Uwezo wake wa kurap na kuandika umepelekea Msamiati kuwa moja ya marapa wanaofanya vizuri zaidi nchini Tanzania na ambaye ana CV ya kufanya kazi na wasanii tofauti tofauti kama Young Lunya, Dayoo na Lody Music. 

Hivi hapa ni vitu 5 ambavyo ulikuwa huvifahamu kuhusu rapa Msamiati: 

1.Maisha Ya Awali 

Jina halisi la Msamiati ni Freddy Benny Mbetwa na amezaliwa mkoani Mbeya huku yeye ni mtoto wa kwanza kwenye familia yao. 

Msamiayi alianza kupenda muziki tangu akiwa mdogo na wakati anakua alikuwa akipenda kusikiliza ngoma za wasanii tofauti kama Albert Mangwair, Solo Thang, Professor Jay na Joh Makini. 

 

2.Kwanini aliamua kujiita Msamiati?

Akiongea kwenye mahojiano ya hivi karibuni Msamiati alidokeza kuwa alipewa jina la Msamiati na mashabiki zake ambao walikuwa wakipenda namna ambavyo anatumia maneno na kucheza na lugha na hivyo kuamua kumpachika jina hilo ambalo analitumia hadi hivi sasa.

 

3.Kuanza Muziki Rasmi Na Kuachia Ngoma Ya Kwanza 

Msamiati alirekodi ngoma yake ya kwanza ya kuitwa Moja Moja chini ya MJ Records ambapo kwa kipindi hicho alikuwa bado mjini Mbeya. 

Mara baada ya kuisikia ngoma hiyo, Marco Charlie ambaye ndiye CEO wa MJ Records alivutiwa na kipaji cha Msamiati na alianza kumpa kazi ya kuandikia wasanii wengine.

Mara baada ya Moja Moja kuingia sokoni, ngoma hiyo ilifanya vizuri na iliweza kupenya kwenye redio kubwa kubwa Tanzania ikiwemo Clouds FM kupitia kwa Adam Mchomvu ha kutokea hapo safari ya Msamiati kwenye kiwanda cha muziki ikaanza. 

 

4.Collabo Za Msamiati

Tangu aanze kufanya muziki, Msamiati ameshafanya kazi na wasanii tofauti tofauti ndani ya Tanzania ikiwemo Joh Makini, Young Lunya, Conboi, Dayoo, Loddy Music na wengineo wengi.

Kwenye mahojiano yake ya hivi karibuni, Msamiati alidokeza kuwa pia ameshafanya kazi na wasanii wengine kutoka Kenya, Uganda na Afrika Kusini na kwamba huenda collabo hizo zikaingia sokoni muda wowote kutokea sasa.

5.Aina Ya Muziki Na Upekee Wa Msamiati

Msamiati anafanya muziki wa rap au Hip Hop na moja ya kitu kinachomtofautisha yeye na marapa wengine ni ubunifu wake wa kuchanganya lugha ya kinyakyusa kwenye muziki wake.

Kupitia ngoma zake kama Unyakyusa Mwingi na Malafyale, Msamiati ameweza kuchanganya Kiswahili na Kinyakyusa na hivyo kumfanya kuwa tofauti na marapa wengine.

Leave your comment