Mario Adokeza Collabo Nyingine Na Ali Kiba


Picha: Instagram
Mwandishi: Charles Maganga

Fundi wa muziki kutoka Tanzania Marioo hivi karibuni ameingia kwenye vichwa vya habari nchini baada ya kudokeza ujio wa collabo mpya kati yake na CEO wa Kings Music Ali Kiba. 

Siku ya Jumapili wawili hao yaani Ali Kiba na Marioo walitumbuiza pamoja kwenye tamasha la “Reloaded” ambalo pia lilisindikizwa na msanii nguli kutoka Nigeria wa kuitwa Ayra Starr. 

Mara baada ya tamasha hilo kumalizika, Marioo alitumia ukurasa wake wa Instagram kudokeza ujio wa ngoma yake mpya na Ali Kiba ambapo aliandika kwa kumsihi Ali Kiba atoe wimbo huo waliofanya pamoja kwani amechoka kukaa na “Hit” ndani. 

“Mfalme Ali Kiba” Dondosha lile banger. Naona kama Nashindwa kuvumilia kukaa na hit ndani” aliandika Marioo kwenye ukurasa wake wa Instagram. Katika ujumbe wake huo Marioo hakutaja jina la ngoma wala tarehe ambayo ngoma hiyo inatarajiwa kuachiwa. 

Ikumbukwe kuwa Marioo na Ali Kiba wameshafanya collabo ya pamoja kwenye “I Miss” ngoma ambayo inapatikana kwenye albamu ya Marioo ya kuitwa “The Kid You Know” ambayo iliachiwa mwishoni mwa mwaka 2022. 

Leave your comment