Marioo Afunguka Baada Ya Kukosa Tuzo Kwenye Tanzania Music Awards 2023

[Picha: Instagram]

Mwandishi-Charles Maganga 

DOWNLOAD LATEST BONGO MUSIC MP3

Msanii wa Bongo Fleva, Marioo hatimaye amefunguka kwa mara ya kwanza baada ya kukosa tuzo kwenye tuzo za Tanzania Music Awards zilizofanyika mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu. 

Marioo ambaye kwa sasa anatamba na toleo lake jipya la albamu yake ya “The Kid You Know” amezungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuondoka patupu kwenye tuzo za mwaka huu. 

Kwenye tuzo hizo ambazo huandaliwa na Baraza La Sanaa La Taifa (BASATA) Marioo alitajwa kuwania vipengele mbalimbali kama Msanii Bora Wa Kiume Bongo Fleva, Wimbo Bora Wa Mwaka, Video Bora Ya Mwaka na vipengele vingi zaidi ambapo Marioo hakushinda katika kipengele chochote. 

Akizungumza hivi karibuni kwenye mahojiano East Africa Radio, Marioo alidokeza kuwa amekubaliana na uamuzi wa waandaaji wa tuzo hizo na kwamba yupo tayari kwa ajili ya tuzo za mwaka ujao. 

“Mimi nawaombea tu wapate mawazo makubwa zaidi wahakikishe kwamba tuzo za mwakani zinaenda vizuri zaidi kwa sababu hata hiyo BET yenyewe naskia kuna makosa madogo madogo yanatokea kwa hiyo sitaki kulaumu na nakubaliana na uamuzi wa kamati yaani” alizungumza Marioo. 

Leave your comment