Cherry Ni Nani ? Kutana Na Nyota Mpya Wa Muziki Kutoka Tanzania.
8 May 2023
[Picha: Instagram]
Mwandishi-Charles Maganga
DOWNLOAD LATEST BONGO MUSIC MP3
Kwenye kiwanda cha muziki ambacho tayari kina Yammi, Zuchu, Anjella na Phina ni rahisi kudhani kwamba kutakuwa na ugumu kwa msanii mwingine wa kike kupenya. Lakini ukiitegea sikio ngoma kama “Closer” “Ole” na “Kiapo Cha Damu” utagundua kwamba bila shaka, Cherry ana kitu cha tofauti na inabidi asikilizwe.
Kwa msanii chipukizi ambaye aliweza kuaminiwa na kampuni kubwa ya M Net mpaka kutengeneza soundtrack EP ya filamu kubwa ya “Love Transfusion” ni dhahiri shahiri kuwa, Cherry ana kitu cha kipekee ambacho kwa sasa hakipo kwenye muziki wa Tanzania.
Jina lake halisi ni Neema Swai na alianza kuimba kanisani pindi akiwa mdogo sana huko mkoani Kilimanjaro. Mapenzi yake ya muziki hayakuishia udogoni kwani mwaka 2009 aliingia rasmi jijini Dar Es Salaam na pamoja na umri wake kuwa mdogo lakini jitihada zake kwenye muziki hazikuacha kuonekana.
Nyota ya Cherry iling’aa zaidi baada ya kushiriki mashindano ya Bongo Star Search mwaka 2020 na kufanikiwa kuingia kwenye kumi bora. Hii ilikuwa ni alama tosha kuwa, ana kipaji cha aina yake kwani mara nyingi huwa si rahisi kutoboa mbele ya majaji kama Madam Ritha, Master Jay na Salama Jabir.
Miezi michache baada ya kushiriki Bongo Star Search, Cherry alisainiwa na B Xtra Records na tangu hapo mambo yameonekana kuwa sukari zaidi kwa upande wake kwani ndani ya lebo hiyo aliweza kuachia ngoma yake ya kwanza ya kuitwa “Ole” na kisha kupata nafasi ya kuachia EP ya “Love Transfusion” kutoka kwenye movie yenye jina hilo pia.
Kama ulikuwa unajiuliza, Cherry anafanya muziki wa aina gani, jibu fupi ni kwamba Cherry anawasikiliza wasanii kama Beyonce na Tems na hivyo kuchagiza yeye kuchanganya Afrobeats na RnB yaani Afro- R&B. Si wasanii wengi wanafanya aina hii ya muziki hasa ukitegemea kwamba kwa sasa muziki wa R&B Tanzania watu wanauchukulia poa.
Kwenye EP ya “Love Transfusion” Cherry amethibitisha kuwa yupo hapa kwa ajili ya kusaidia kurudisha tena hadhi, heshima na ushawishi wa muziki wa R&B nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Mwisho, itoshe kusema, Cherry ni wa tofauti. Hajaribu kuwa mpwani kwa kufanya Baibuda, Hana haraka ya kwenda “international” kwa kulazimisha Amapiano lakini badala yake amejikita kutengeneza aina yake ya muziki ambayo ni ya tofauti na bila shaka itamuweka “Closer” zaidi na mashabiki wake.
Leave your comment