Uchambuzi : Albamu Ya Keysha "Mwangaza"

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram

Kwa sasa watanzania na wana Afrika Mashariki wanasikiliza kiasi cha kusaza albamu mpya ya Keysha ya kuitwa Mwangaza, albamu ambayo imeundwa na ngoma 8 za moto na bila shaka uhodari wa Producers kama Kimambo, Aloneym, Cookie Dady na Bob Manecky umechagiza kazi hii ya Keysha kuwa maridadi sana.

Ili kutumulikia Mwangaza, Keysha aliamua kugawana kipaza sauti na wasanii kama Ali Kiba, Kusah, Frida Amani pamoja na Christian Bella ambao kwa pamoja wameweza kutuletea Keysha yule ambaye wengi walikuwa wakimngoja. Kwenye albamu yake hii, Keysha katuletea Bongo Fleva safi, mashahiri yasiyo na ukakasi lakini bila matata yoyote, Keysha ameweza kuangazia kuhusu mapenzi na maisha kwa ujumla kwa namna tofauti tofauti katika albamu hii.

Huu hapa ni uchambuzi mfupi wa albamu ya Keysha ya kuitwa Mwangaza :

Beautiful Ft Ali Kiba

Hakukuwa na kibao kingine kizuri zaidi cha kufungua albamu zaidi ya Beautiful, kibao ambacho ndani yake Ali Kiba anatumia muda mwingi sana kumsifia na kumpa Keysha maua yake. Muingiliano mzuri wa sauti umepamba vilivyo ngoma hii na kama unapenda Bongo Fleva "Pure" basi hii ni kwa ajili yako.

https://www.youtube.com/watch?v=HYkQSnTM0hs

Sikinai

Kwenye Sikinai Keysha, anakuwa mkali kidogo kimashahiri lakini Utamu wa sauti yake unabaki palepale. Humu ndani Keysha anaapa kumlinda mpenzi wake kwa gharama zozote zile ili asichukuliwe na mwingine huku akitamba kuwa "hatosheki" wala "hakinai" chochote kutoka kwa mpenzi wake.

https://www.youtube.com/watch?v=7YRMMTwOGo8

Mwangaza Ft Christian

Bob Manecky, amefanya mengi ya kushtusha kwenye "Mwangaza". Keysha kwenye wimbo huu akisaidiwa na Christian Bella, anatoa tumaini na faraja kwa watu ambao wamekata tamaa. Kwenye ngoma hii, Christian Bella ameleta sauti yake  mujarab huku Keysha akipamba mkwaju huu na mashahiri mazuri ya kutia moyo.

https://www.youtube.com/watch?v=J36aI9Z4BGI

Darling

Unapenda kucheza? Kama ndio, basi huu mkwaju wa kuitwa Darling utaupenda mno. Ukisikiliza ngoma hii utatabasamu kutokana na namna ambavyo Keysha ameweza kutengeneza ngoma yenye vibe la dansi lakini akiiremba ngoma hiyo kwa misemo, nahau na tamathali za semi ambazo zitakuacha mdomo wazi.

https://www.youtube.com/watch?v=hrxWCQP4qbQ

Wanje Ft Kusah

Ukisikiliza ngoma hii utagundua namna ambavyo Kusah ameweza kumvuta Keysha mpaka kufanya muziki wa "new school" ambao vijana wengi sasa bila shaka watapenda. Gitaa matata la Cookie Dady, mashahiri ya kusisimua ya Kusah na kiitikio kilichojaa uraibu mkubwa, kimependezesha mno ngoma hii

https://www.youtube.com/watch?v=CELdLEQI3s0

Matamu

Kwenye Matamu, utapenda namna ambavyo Keysha amezungumzia na kusifia utamu wa mapenzi bila kutumia matusi au lugha tata. Katika kipindi hiki ambacho wapendanao wanaelekea kwenye msimu wa Valentine hii ni ngoma sahihi kabisa kuisikiliza

https://www.youtube.com/watch?v=9PBcEXha9to

Ni Wako Ft Frida Amani

Frida Amani amewakilisha vyema tasnia ya Hip Hop kwenye album hii kupitia Ni Wako. Mirindimo, mipangilio ya sauti na midondoko ya kwenye ngoma hii inatukumbusha Keysha wa zamani ambaye alitamba na ngoma kama Uvumilivu.

https://www.youtube.com/watch?v=TuPGS1k-ddc

Tulia

Huhitaji Shahada ya Chuo Kikuu kufahamu kwamba Tulia, ni moja kati ya ngoma ambazo Keysha ameonesha uhodari wake katika utunzi wa mashahiri.

Tulia ni aina ya ngoma ambayo unapaswa umsikilizishe mtu ambaye ana sonona na anateswa sana na mapenzi.

https://www.youtube.com/watch?v=5xuOo8mKzpA

Leave your comment