Diamond Platnumz 'Chitaki', 'Pita Huku' Dulla Makabila Na Ngoma Zingine Zinazotamba Tanzania Wiki Hii
6 January 2023
[Picha: Instagram]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram
Katika wiki hii ya kwanza ya mwaka 2022, wasanii tofauti tofauti kutoka Tanzania wameendelea kuonesha ubabe wao katika kiwanda cha muziki kutokana ngoma zao kusikilizwa mitaani na kufanya vizuri kwenye majukwaa mbalimbali ya kusikilizia muziki.
Kuanzia kwenye Singeli, Bongo Hip Hop mpaka Bongo Fleva, zifuatazo ni ngoma tano ambazo zinafanya vizuri zaidi Tanzania kwenye mtandao wa Youtube kwa wiki hii :
Pita Huku - Dullah Makabila
Wiki hii bendera ya muziki wa singeli imeweza kupeperushwa vyema na Dulla Makabila kupitia ngoma yake ya Pita Huku ambayo ndani yake Dulla Makabila amekemea mambo mbalimbali kama kula rushwa, kukosa uaminifu kwenye ndoa na mambo mengine mengi.
Mashabiki wengi wamependa ubunifu wa Makabila kwenye ngoma na video hii ambayo kufikia sasa imeshatazamwa mara Milioni 2.2 Youtube.
Chitaki - Diamond Platnumz
CEO wa WCB, Diamond Platnumz aliamua kuufunga mwaka 2022 kwa kuachia Chitaki, ngoma ambayo kwa sasa inapamba mitaa pamoja na klabu mbalimbali za starehe Tanzania. Kwenye Chitaki Diamond Platnumz anachanganya Bongo Fleva pamoja Amapiano kutengeneza mdundo mpya ambao una lengo la kuwachezesha mashabiki.
Huyu Hapa - Mbosso
Kutoka kwenye EP yake ya Khan, Mbosso hivi karibuni aliachia video ya Huyu Hapa ambapo ndani yake Mbosso anavaa uhusika wa mfalme ambaye anampamba malkia wake kwa kumuimbia maneno mazuri. Video ya Huyu Hapa imefanyika huko Afrika Kusini na video ya pili kutoka kwenye EP ya Khan.
Rose Muhando - Secret Agenda
Malkia Rose Muhando ameendelea kufanya vizuri na ngoma yake ya Secret Agenda ambayo imekuwa ni gumzo sio tu mtaani lakini pia imekuwa maarufu huko Tiktok. Kwenye kazi hii utapenda mashahiri ya Rose Muhando, ubunifu uliotumika kwenye video pamoja na mitindo ya dansi iliyotumika
Puuh - Billnass Featuring Jay Melody
Zimepita takriban wiki tatu tangu Billnass aachie Puuh ngoma ambayo amemshirikisha Jay Melody na kufikia sasa tayari ngoma hii imeshatazamwa mara Milioni 2.7 kwenye mtandao wa Youtube, kitu ambacho ni nadra sana kutokea kwenye muziki wa Hip hop Tanzania.
Leave your comment