Wasanii Bora Chipukizi Kutoka Tanzania Kwa Mwaka 2022

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram

Moja ya vitu ambavyo vimechagiza Bongo Fleva na muziki wa Tanzania kukua kwa ujumla ni pamoja na vipaji vipya ambavyo kila mwaka huchanua na kutuletea midundo mipya, aina mpya ya uandishi wa ngoma na vitu vingine vizuri sana.

Mwaka 2022 haukuwa mwaka wa tofauti kutokana na kwamba tangu Bongo Fleva ianze kushika mizizi mwishoni mwa miaka ya 90, mwaka huu pia kama ilivyo miaka mingine, wasanii wengi wapya wamezaliwa ambao kwa miaka ya baadae wanatarajiwa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Wafuatao ni wasanii bora chipukizi Tanzania kwa mwaka 2022.

Kontawa

Kontawa alipeperusha vyema bendera ya Hiphop kwa mwaka 2022 kupitia ngoma yake ya Champion ambaye ilitikisa kila kona ya nchi. Champion ni ngoma ambayo Kontawa anazungumzia kuhusu uhalisia na changamoto za maisha ya mtaani.

Champion Remix ambayo alimshirikisha Harmonize pia iliweza kufanya vizuri sana na kutokana na ngoma hiyo, Kontawa alipata nafasi ya kushiriki kwenye matamasha makubwa ya muziki Tanzania ikiwemo Muziki Mnene.

Micky Singer

Micky Singer amepata umaarufu mkubwa mwaka huu kutokana na ngoma yake ya Wanijue ambayo ndani yake ndio kuna ule mstari pendwa wa "Yani na mimi ipo siku moja. Nikipata pesa nami ninunue sabufa", mstari ambao umekuwa maarufu sana kwenye Tiktok na Instagram mwaka huu.

"Sitaki Ndoa" ni ngoma nyingine ambayo ilimfanya Micky Singer aweze kuwika zaidi 2022 kiasi cha kuweza "Kuweka Maneno" kwenye tamasha la Fiesta 2022.

Vanillah 

Kama unapenda wimbo wa Ali Kiba wa kuitwa "Utu" basi bila shaka utampenda pia Vanillah ambaye ni mwandishi wa ngoma hiyo ambayo ilimpatia Ali Kiba ushindi mnono kwenye tuzo za Tanzania Music Awards 2022 na baada ya kufanya kazi hiyo kubwa kwa mwaka huu Vanillah ametambulishwa rasmi kuwa msanii wa Kings Music.

EP yake ya kuitwa Listen To Me imependwa vilivyo na mashabiki hasa ukuzingatia uandishi wa aina yake ambao unaonekana  kupitia ngoma kama Unanisitiri

Mavokali

Mwaka huu Mavokali, alipeperusha vyema bendera ya Tanzania duniani baada ya kuachia Commando ngoma ambayo ilisambaa kwa kasi, sio tu Tanzania, lakini pia kwenye nchi kama Saudi Arabia, Columbia, Peru na nyingine nyingi huku DJ Khaled nae alionekana akicheza ngoma hiyo.

Rayvanny aliamua kunogesha ngoma hiyo kwa kudandia kwenye remix ya ngoma hiyo, kitendo ambacho kimeongeza thamani kwenye muziki wa Mavokali.

Mary G

Kwa mwaka 2022, Mary G alitupatia ngoma mbalimbali kama Love, Nishazama pamoja na Hiari Yangu na kutokana na juhudi zake nyota huyu alitajwa kuwania tuzo mbalimbali.

Kwenye Tanzania Music Awards, Mary G, alitajwa kuwania kipengele cha msanii bora chipukizi, kipengele ambacho alikipoteza kwa Phina huku kwenye Bongo Music Awards akitajwa pia kuwania katika kipengele hicho hicho cha msanii bora chipukizi akiwa anachuana na nyota wengine kama Phina, Anjella na Abby Chams.

Haitham Kim

Ukiweka kando muonekano wake wa "kistaa", juhudi za Haitham Kim katika kusogeza muziki wake zinatosha kusema kwamba miaka michache ijayo, atakuwa tishio kubwa sana.

Mwaka huu Haitham Kim amejing'arisha na ngoma mbalimbali ikiwemo "Ex Mtamu", mkwaju ambao pamoja na kwamba una mashairi ya kiutu uzima kidogo lakini hauchoshi kusikiliza.

 

Platform TZ

Mwaka huu Platform TZ ametuburudisha na mengi sana lakini kubwa kabisa lililochagiza maelfu ya watu kumpa sikio ni ngoma yake ya "Fall" ambayo amemshirikisha Baddie, Marioo.

Sauti yake, midondoko pamoja na mashairi yake mazuri pia vilimshawishi Barnaba Classic kumuamini na kumshirikisha kwenye ngoma namba 18 ya kuitwa She Got One ambayo pia Ziddy Value ameshirikishwa.

 

Leave your comment