Collabo 10 Bora Tanzania 2022
20 December 2022
[Picha: Instagram]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram
Tangu kuanzishwa kwa muziki wa Bongo Fleva kwenye miaka ya 1990, suala la wasanii wawili au zaidi kushirikiana ili kutengeneza ngoma ya pamoja limekuwa likitiliwa maanani sana.
Kwa miaka ya hivi karibuni sio tu kwamba collabo zinafanyika ndani ya nchi lakini pia wasanii wamekuwa wakishirikisha wasanii wa mataifa mengine kama Nigeria, Kenya, Uganda na mataifa mengine na kwa mwaka 2022 mambo yameendelea kuwa sukari sana kwenye upande huo wa collabo.
Hizi hapa ni collabo kali kutoka Tanzania kwa mwaka 2022.
Naogopa - Marioo Featuring Harmonize
Waswahili husema mahafali wawili hawawezi kukaa zizi moja lakini kupitia "Naogopa" Marioo na Harmonize waliweza kukanusha msemo huo. Huu ni wimbo ambao kwa wengi ulijizolea umaarufu mkubwa sana kutokana na kiu iliyokuwepo ya kutaka kuwasikia Marioo na Harmonize.
Video ya Naogopa ni moja kati ya video zilizotazamwa zaidi Tanzania kwa mwaka 2022 kwani kufikia sasa imeshatazamwa zaidi ya mara Milioni 16.
Nidhibiti - Jux Featuring Zuchu
Kwenye ngoma hii Zuchu aliweza kuipaka rangi vizuri Baibuda kwa namna ambayo sauti yake iliweza kurandana na miondoko ya R&B ya Jux. Ngoma hii ilikuwa ni "Hit" kabla ya kuachiwa kwake rasmi huku wengi wakionekana kukipenda zaidi kiiitiko cha wimbo huo.
Marry Me - Barnaba Classic Featuring Marioo
Akiwa kwenye mahojiano na Lil Ommy Barnaba alikiri kuwa wazo la ngoma ya Marry Me lilikuwa sio la kwake bali ni la Marioo na Abbah huku wimbo huo ukiwa umerekodiwa kuanzia saa 4 usiku mpaka 1 asubuhi.
Marry Me imepambwa na sauti nzuri ya Marioo ambayo unaweza ukahisi analilia mapenzi lakini badala yake anamsifia mpenzi wake kwa namna ambavyo hashikwi na hasikii lolote kama "Mkate Kwenye Tea"
Mtasubiri - Diamond Platnumz Featuring Zuchu
Mtasubiri ni moja kati ngoma ambazo zilizofanya vizuri sana kwa mwaka 2022 na ngoma hii ilitoka katika kipindi ambacho tetesi za kwamba Diamond Platnumz na Zuchu ni wapenzi. Kwa sasa video ya "Mtasubiri" imeshatazamwa mara Milioni 23 huko Youtube
Sio Kwa Ubaya - Mwana FA Featuring Harmonize.
Ukisikiliza Sio Kwa Ubaya, sio tu kwamba utapata burudani lakini pia utapata mawaidha na darasa la bure kabisa kutoka kwa Mwana FA huku Harmonize akiwa amepamba ngoma hiyo kwa kiitikio kizuri.
Kwa mujibu wa Mwana FA, mara ya kwanza yeye alikuwa amefikiria kumshirikisha Maua Sama lakini baada ya kumsikilizisha ngoma hii Ommy Dimpoz, yeye ndiye alishauri Harmonize ashirikishwe badala ya Maua Sama.
Love - Zuchu Featuring Adekunle Gold
Baada ya Nobody ya mwaka 2020, Zuchu kwa mara nyingine alionesha juhudi zake za kupenya kwenye soko la Nigeria kupitia Love, ngoma ya Afrobeats ambayo ilikuna watu wengi sana.
Champion - Kontawa Featuring Nay Wa Mitego
Hii ni moja kati ya ngoma bora za Hiphop kutoka Tanzania kwa mwaka 2022 ambapo ndani yake Kontawa alizungumzia uhalisia wa maisha ya mtaani na changamoto zake, kitu ambacho kiligusa watu wengi sana ikiwemo Harmonize ambaye mara baada ya ngoma hii kutamba aliamua kujumuika na Kontawa kwa ajili ya remix
Puuh - Billnass Featuring Jay Melody
Tangu kuachiwa kwake Puuh imekuwa ni ngoma pendwa baina ya mashabiki na hii ni kutokana na mashahiri mepesi kabisa ya Billnass lakini kubwa kabisa kiitikio cha aina yake cha Jay Melody ambacho kilipamba ngoma hii.
Fall - Platform TZ featuring Marioo
Fall ni moja kati ya ngoma bora kwa mwaka 2022 ambapo ndani yake Platform na Marioo wanaamua kumwagia binti wa kike kwa kuonesha sifa zake.
Melody pamoja na namna ambavyo Marioo amefungua ngoma hii unaweza ukadhani huu ni wimbo wa maumivu ya mapenzi lakini badala yake hii ngoma nzuri ya mapenzi ambayo kwa mara nyingine imemtambulisha vyema Platform TZ
Nitongoze - Rayvanny Featuring Diamond Platnumz
Kama unatafuta wimbo kwa ajili ya kucheza na kupandisha mizuka ukiwa club basi ngoma hii ya Nitongoze itakufaa sana kutokana na namna ambavyo Rayvanny na Diamond Platnumz wameweza kwa mara nyingine wameweza kutengeneza mdundo wa tofauti.
Leave your comment