Uchambuzi : Vitu 5 Vya Kipekee Na Vya Kufahamu Kuhusu Albamu ‘The Kid You Know’ Ya Marioo

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram

Siku ya Ijumaa mwanamuziki Omari Mwanga maarufu kama Marioo alitetemesha Tanzania  baada ya kuachia albamu yake ya kuitwa The Kid You Know ambayo kwa muda mrefu sasa ilikuwa inasubiriwa mno na mashabiki wa muziki.

Kwa mara ya kwanza Marioo alitangaza  kuhusu albamu yake ya The Kid You Know kwenye usiku wa Tuzo za muziki Tanzania ambazo zilifanyika mwezi Aprili na mwishoni mwa mwezi Novemba ndipo alipoachia tracklist ya albamu hiyo ambayo imesheheni ngoma 17 za moto huku akiwa amewashirikisha wasanii tofauti tofauti kama Rayvanny, Loui, Ali Kiba, Dunnie kutokea Nigeria na wengineo.

Kwa sasa "The Kid You Know" imekuwa ni albamu pendwa baina ya mashabiki huku ngoma kama "Siwezi", "I Miss" pamoja na "Lonely" zikiwa zinafanya vizuri zaidi. Haya ni mambo matano ambayo unatakiwa kuyafahamu kuhusu albamu hiyo.

Aina Ya Muziki

Mashabiki wengi huwa hawana shaka na kipaji cha Marioo na hii ni kutokana na uwezo wake wa kufanya aina tofauti tofauti za muziki na kwenye "The Kid You Know" Marioo ameendelea kuthibitisha hilo. Ndani ya albamu hii Marioo amefanya Amapiano, Bongo Fleva, Kizomba, R&B bila kusahau Bongo Fleva.

Hii inathibitishwa na ngoma ya 'Siwezi' ambayo Marioo amefanya Bongo Fleva huku kwenye ngoma ya 'Lonely' akiwa amefanya Amapiano.

https://www.youtube.com/watch?v=ef3VwKm2OgU

 

Maudhui Ya Albamu

Ndani ya "The Kid You Know" Marioo ametumia sauti yake kuzungumzia sana kuhusu mapenzi. Kwenye ngoma kama "I Miss You" na "Anisamehe"pamoja na" Lonely" Marioo anazungumzia kuhusu maumivu yatokanayo na mapenzi huku kwenye ngoma kama "Naogopa" pamoja na "Mi Amor" msanii huyo anaonesha kukoshwa na kufurahia zaidi  huba.

Katika albamu hii pia, Marioo anatuhadithia kuhusu maisha yake hasa kwenye kibao cha  "My Life", ngoma ambayo inafungua albamu.

https://www.youtube.com/watch?v=nBmiP5OWPgw

Uthubutu Wa Marioo

Wengi tunamfahamu Marioo kama msanii wa Bongo Fleva ambaye mara zote amekuwa akijiachia sana kwenye muziki huo wenye asili ya Tanzania pamoja na muziki wa Amapiano. Lakini kwenye albamu hii ya "The Kid You Know" Marioo anathubutu kupanua uwanja wake wa kisanaa kwa kufanya Afrobeats kwenye ngoma ya Lagalaga ambayo amemshirikisha "Dunnie"

Tofauti na collabo nyingi za baina ya wasanii wa Tanzania na Nigeria, kwenye Lagalaga Marioo anadandia kwenye Afrobeats ya taratibu ambayo haimlazimishi msikilizaji kucheza bali inachagiza msikilizaji arahani mashahiri pamoja na sauti nzuri ya Marioo.

https://www.youtube.com/watch?v=jfYrTtiwSYc

Uandishi Wa Nyimbo

Pamoja na kwamba ngoma nyingi za kwenye "The Boy You Know" zinahusu mapenzi lakini Marioo amejitahidi kuzungumzia mapenzi katika pande tofauti tofauti.

Wakati kwenye "Naogopa" Marioo anaonesha namna gani ana hofu ya kuachwa na mpenzi wake, kwenye "Anisamehe" anaomba msamaha ili mwenzi wake amrudie.

Uandishi wake pia unaonekana kwenye ngoma ya Ngoma Ya "Lonely" akiwa na Loui, ambapo kwa ufundi mkubwa Marioo anaelezea huzuni, upweke, hofu na majuto aliyonayo kwa kutumia beat kali la Amapiano kitu ambacho hakijazoeleka sana kwani ngoma nyingi za Amapiano huwa zina lengo la kuchangamsha.

https://www.youtube.com/watch?v=ef3VwKm2OgU

Collabo Za Kwenye Albamu

Marioo bila shaka amechagua wasanii sahihi wa kupamba albamu hii. Ukisikiliza ngoma ya  "I Miss" utagundua kwamba kuna muingiliano mzuri sana wa kisanaa kati ya Marioo na Ali Kiba ambapo Ali Kiba ameshughulika zaidi kupamba ngoma hiyo na sauti yake nyepesi huku Marioo akiwa ametumia mashahiri ya aina yake ili kufanya ngoma hiyo iweze kutaradadi.

Collabo nyingine bora kwenye albamu hiyo ni pamoja na Naogopa ambayo kashirikishwa Harmonize pamoja na Lagalaga ambayo Marioo kamshirikisha Dunnie.

 

Leave your comment