Konde Gang Waomba Radhi Kutokana Na Ngoma Ya "Weed Language"

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram

Lebo ya Konde Music Worldwide ambayo inamilikiwa na Rajab Kahali maarufu kama Harmonize hivi karibuni imetikisa vyombo vya habari nchini Tanzania baada ya kuomba radhi kutokana na maudhui ya ngoma ya hivi karibuni ya Harmonize ya kuitwa Weed Language.

Kabla ya waraka huu wa kuomba radhi siku chache zilizopita, Kamishna Mkuu Wa Kupambana Na Dawa Za Kulevya, Gerald Kusaya alionekana kutopendezwa na maudhui ya wimbo huo na kutoa onyo kwa wasanii wote wanaohamasisha matumizi ya mihadarati.

Saa chache tangu kutolewa kwa kauli hiyo, uongozi wa Konde Gang umetoa waraka ambao ndani yake waliomba radhi kutokana na maudhui ya wimbo huo na kudokeza kwamba lengo la Konde Gang lilikuwa jema tu kwani walitaka kupanua muziki wa Tanzania nje ya nchi.

"Uongozi wa konde music worldwide unaomba radhi kutokana na maudhui ya wimbo tulioutoa hivi karibuni unaoitwa 'WEED LANGUAGE'. Wimbo huu ulilenga kupanua na kukuza muziki wetu nje ya mipaka ya nchi yetu

Lakini tafsiri ya maudhui ya wimbo huo yanakiuka maadili utamaduni, mila na desturi pamoja na miongozo ya mamlaka za serikali nchini

Kutokana na kadhia iliyosababishwa na maudhui ya wimbo huo tunaomba radhi na tunahaidi kuuondoa wimbo huo kwenye mitandao yote ya kijamii.

Pia tunahaidi kuboresha nyimbo zetu ili ziendane na utamaduni wetu pamoja na miongozo ya mamlaka ya serikali.

Imetolewa na uongozi wa konde music worldwide" ulisomeka ujumbe huo.

Kando na wimbo huu wa Weed Language, ngoma nyingine kutoka Tanzania ambao ulipata changamoto kutokana na maudhui yake ni video ya Mtasubiri ya Diamond Platnumz na Zuchu.

 

 

Leave your comment