Uchambuzi : Ngoma 10 Kali Kwenye Albamu Mpya Ya MansuLi "Love Life" 

Download FREE Mp3 Music by MansuLi on Mdundo.com

Kwenye kipindi ambacho kiwanda cha muziki nchini Tanzania kimetawaliwa na Bongo Fleva, Baibuda pamoja na Amapiano, rapa mashuhuri kutokea nchini humo MansuLi anajitokeza kama mkombozi wa muziki wa Hip Hop kwa kuachia albamu yake mpya kabisa ya kuitwa Love Life. 

Tofauti kabisa na kwenye albamu yake ya kwanza ya kuitwa Kina Kirefu ambayo ilitoka mwaka 2007, kwenye kazi hii mpya MansuLi anaachana kabisa na rap ya kiunaharakati na badala yake kwenye ngoma zote 20 za kwenye albamu hii MansuLi anaelezea dhana nzima ya mapenzi. 

Kwenye Love Life, MansuLi amejikita kwenye kuelezea zaidi kuhusu utamu, changamoto pamoja na karaha zitokanazo na mapenzi na bila shaka kupitia albamu hii MansuLi ni kama amejifufua upya kisanaa. Kwenye makala hii tutaangazia kwenye ngoma 10 kutoka kwenye albamu hiyo : 

Love Life Featuring Fetty Sley 

MansuLi alifanya uamuzi sahihi kabisa kwa kuweka mkwaju huu kama ngoma namba 1 kwenye albamu kwani humu ndani MansuLi anatuhadithia kuhusu historia yake ya mapenzi kuanzia akiwa shule ya msingi mpaka sekondari. Sauti tamu ya Fetty Sley imechagiza ubora wa ngoma hii. 

Madoido Part 1 Featuring G Nako 

Kwenye ngoma hii utapenda namna ambavyo sauti nzuri ya G Nako imepamba kiitikio cha wimbo huu ambao ndani yake Mansuli anavaa uhusika wa mwanamuziki ambaye anajaribu kumshawishi binti ili awe mpenzi wake lakini binti huyo anaonekana kuwa na maringo na kutokuwa na uhakika kuhusu maamuzi yake. 

Mishe Mishe Featuring Chiku Keto 

Mishe Mishe ni ngoma ambayo ina kiitikio chepesi zaidi kwenye albamu lakini mashahiri yake ni mazito na yanaweza kukufanya ushangazwe na hazina kubwa ya uandishi aliyokuwa nayo MansuLi. Stori nzima ya wimbo huu ambapo Mansuli anahadithia namna ambavyo alikutana mwenza wake kwenye "Mishemishe" bila shaka imeonesha ubunifu wake kwenye uandishi. 

Tustarehe Featuring Aveli & Chege 

Kwenye ngoma hii Mansuli anajaribu kupita kwenye beat ya Hip Hop ya kisasa lakini uandishi wake wa zama za kale pamoja na kiitikio cha aina yake kutoka kwa Chege kimefanya ngoma hii isheheni vionjo vya Hiphop vya miaka 90. Ngoma hii imetayarishwa na S2kizzy. 

Siku Yetu Featuring Mapanchi BMB 

Mara tu utakaposikiliza ngoma hii, fikra zako zitakukumbusha ngoma ya Vacation ya kwake Ommy Dimpoz.  Siku Yetu ni ngoma mahususi ambayo unatakiwa kuisikiliza na mpenzi wako pindi mkiwa kwenye mapumziko au honeymoon. 

Usiondoke Featuring Nuru The Light 

Usiondoke ni ngoma ya kwanza kwenye albamu ambayo MansuLi anatuonjesha maumivu yanayotokana na mahusiano. Humu ndani MansuLi anakiri makosa na kuomba msamaha kutokana na kumkosea mpenzi wake na kwa wale wote waliokuwa wanatamani kusikia sauti tamu ya Nuru The Light, basi ngoma hii pia imelenga kukata kiu yao. 

Baby Mama Featuring Dully Sykes

Maumivu ya mapenzi ya MansuLi yameendelea kusikika pia kwenye Baby Mama, ngoma ambayo ndani yake MansuLi anatangaza kumuacha mpenzi wake kutokana na kufanyiwa "visa" na mpenzi wake huyo. 

Sina Gari Featuring Chemical 

Ni ngoma nyingine kali kutoka kwenye albamu hii ambapo MansuLi anahadithia  jinsi ambavyo alimkosa binti aliyekutana naye mgahawanivkwa sababu tu hana gari. Stori nzima ya ngoma hii bila shaka itakufanya upate shauku ya kusubiri video yake. 

Shabiki Remix Featuring Sabrina & One Six

Shabiki Remix ni ngoma nyingine ya aina yake ambayo MansuLi anatoa stori kuhusu namna ambavyo shabiki yake ambaye mara ya kwanza alimuona kwenye TV alimpenda. Ngoma hii imejaa vionjo vya Bongo Hip Hop ya miaka 90. 

Usiku Mmoja Featuring Zafa 

Hii ni ngoma ambayo MansuLi anaelezea majuto yake baada ya kufanya makosa nyakati za usiku ikiwemo kumsaliti mpenzi wake. Ngoma hii imenogea zaidi kutokana na ukweli kwamba verse ya kwanza ina stori tofauti kabisa na stori ya verse ya 2. 

Leave your comment