Ngoma Tano Bora Zilizopelekea Kukua Kwa Muziki Wa Singeli Wa Tanzania

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram

Kwa sasa singeli ni moja kati ya aina ya muziki inayopendwa sana nchini Tanzania ambapo kwa miaka ya hivi karibuni wasanii wa singeli wamekuwa wakipata nafasi ya kutumbuiza kwenye majukwaa makubwa ya muziki Tanzania, wasanii hao pia wamekuwa wakipata dili za ubalozi wa kampuni mbalimbali huku wasanii wa Bongo Fleva kama Zuchu, Harmonize, Nandy, Rayvanny na wengineo pia wameonekana kutoa nyimbo za singeli.

Kwa sasa nchini Tanzania wanamuziki kama Dulla Makabila, Man Fongo, Kinata Mc na wengineo wamepata umaarufu mkubwa sana kutokana na muziki huo. Zifuatazo ni ngoma 5 ambazo zimechagiza muziki wa Singeli, kuwa muziki pendwa baina ya mashabiki Tanzania

 

Hainaga Ushemeji - Man Fongo

Man Fongo aliweza kutikisa spika za watanzania mwaka 2016 baada ya kuachia "Hainaga Ushemeji" ngoma ambayo iliweza kupata umaarufu mkubwa sio tu maeneo ya uswahilini ambapo muziki wa Singeli ulianzia lakini pia katika maeneo mbalimbali ya nchi na kwa rika mbali mbali.

Hii ni ngoma ambayo pia, ilimuwezesha Man Fongo kubeba tuzo ya msanii bora chipukizi kwenye tuzo za EATV Awards zilizofanyika mwaka 2016.

https://www.youtube.com/watch?v=gkLL3AJ5Y_I

Makabila - Dullah Makabila.

Kupitia wimbo huu, Dulla Makabila alidhihirisha kuwa unaweza ukaimba singeli na bado ukafikisha ujumbe fulani katika jamii na watu wakapenda. Makabila ni wimbo ambao ulipokelewa kwa mikono miwili na mashabiki kutokana na uandishi mzuri wa Dulla Makabila na ni wimbo ambao ulifungulia njia, ngoma nyingine za, singeli kuchezwa zaidi kwenye vyombo vya habari.

https://www.youtube.com/watch?v=F_A6kmF0IwE

Wanga Wabaya - Meja Kunta Ft Lavalava

Hii ni ngoma ambayo ilionesha kuwa muziki wa Singeli ukiunganishwa na Bongo Fleva, ngoma inakuwa ni sukari sana. Kupitia ngoma hii wengi waliweza kumfahamu zaidi Meja Kunta na hii ni moja ya ngoma ya singeli ambayo imeshatazamwa sana kwenye mtandao wa YouTube, kwani kufikia sasa imeshatazamwa mara Milioni 6

https://www.youtube.com/watch?v=SV1ra6fchW0

Nyumba Ndogo - Zuchu

Kupitia "Nyumba Ndogo" Zuchu aliweza kushawishi wasichana wengi kupenda singeli lakini pia aliweza kuuepeleka muziki wa singeli kimataifa zaidi kwani wakati anatumbuiza kwenye onesho la Africa Day Concert huko nchini Nigeria  miezi michache nyuma, Zuchu alitumbuiza ngoma hii.

Nyumba Ndogo pia imeweka rekodi ya kuwa ngoma ya Singeli iliyotazamwa zaidi kwenye mtandao wa YouTube kwani kufikia sasa imeshatazamwa mara Milioni 23 kwenye mtandao huo.

https://www.youtube.com/watch?v=KsU31FyvFxY

Mwanaume Mashine - Msaga Sumu

Pamoja na ngoma hii kuzua utata pindi ilipotoka lakini bila shaka kupitia ngoma hii Msaga Sumu aliweza kuileta aina mpya ya singeli ambayo ilikuwa na utofauti mkubwa na ile iliyozoeleka kwani ngoma hii ilikuwa na mashahiri mepesi na ya tofauti, ngoma ilikuwa fupi tofauti na singeli za zamani.

Ngoma hii iliashiria mwanzo mpya wa muziki wa Singeli Tanzania, kwani ilikuwa tofauti sana na singeli zilizozoeleka kipindi hicho.

https://www.youtube.com/watch?v=BH2zxc3Amkg

Leave your comment