Wasanii Watano Watanzania Ambao Wanatarajia Kuachia Albamu Mwaka Huu

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pakua Ngoma Zake Mac Voice Bila Malipo Kwenye Mdundo

Itoshe kusema kuwa mwaka 2022 tumebarikiwa kupata albamu tofauti tofauti ambazo zimeweza kuchangamsha kiwanda cha Bongo Fleva. Wasanii kama Beka Flavour ambaye ameachia "Last Born", Ibraah ambaye ameachia "King Of New School" pamoja na Balaa MC ambaye aliachia albamu yake ya singeli ya kuitwa 26 kipaji bila shaka wameweza kuupamba mwaka huu kwa burudani kali.

Kando na wasanii kuna wasanii wengine ambao kupitia mahojiano na vyombo vya habari au mitandao ya kijamii walitangaza kuachia albamu zao ndani ya mwaka huu. Wafuatao ni wasanii watano kutoka Tanzania ambao wanatarajia kuachia albamu mwaka huu.

Barnaba

Mhitimu huyu wa THT anatarajiwa kutetemesha Bongo Fleva ifikapo Julai 28 mwaka huu na albamu yake ya kuitwa "Love Sounda Different" ambayo ametanabaisha kuwa itakuwa na ngoma 18 ambazo zote ameshirikisha wasanii wenzake wa ndani na nje ya Tanzania. Albamu hii ni maadhimisho ya miaka 18 ya Barnaba kwenye muziki wa Tanzania na alitanabaisha kuwa atachukua asilimia 18 ya mapato yote ya albamu na kuwapa watu wenye mahitaji.

Marioo

Wakati akiwa anatoa hotuba fupi wakati anapokea tuzo kwenye usiku wa tuzo za Tanzania Music Awards 2022 Marioo akiwa jukwaani alitangaza kuwa anatarajia kuachia albamu mwaka huu ya kuitwa The Boy You Know. Tangu hapo mashabiki wamekuwa wakisubiria kwa hamu albamu hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kutoka kwa mtoto wa "Mama Amina"

Rosa Ree

Tetesi kuhusu albamu ya Rosa ree zilianza kusambaa tangu mwaka jana baada ya msanii huyo kutangaza kuwa albamu yake imeshakamilika lakini mwezi Januari mwaka huu msanii huyo aliahirisha kuiachia na kusema kuwa ataileta sokoni miezi kadhaa mbele. Ikumbukwe kuwa katika albamu hiyo Rosa ree alidokeza kuwa msanii Chemical pia  atakuwepo.

Zuchu

Zuchu mara kadhaa kupitia akaunti yake ya Instagram amekuwa akidokeza kuwa yuko mbioni kuachia albamu, ambayo inatarajiwa kuwa ya kwanza kutoka kwake. Ikumbukwe kuwa kufikia sasa Zuchu ameachia EP moja ya kuitwa "I Am Zuchu" pamoja na project mbili ambazo ni Side 2 Side na 4.4.2

Jux

Akiwa anafanya mahojiano na Lil Ommy kwenye Podcast miezi kadhaa nyuma , Jux alitanabaisha yuko mbioni kuachia albamu yake ya pili ya kuitwa "King Of Hearts" ambayo inatarajiwa kuachiwa miezi kadhaa huko mbeleni.

Leave your comment