Chidi Benz Azungumzia Albamu Yake Kupokewa Vizuri Licha ya Wasanii Kukosa Kumuunga Mkono

[Picha: Mpasho]

Mwandishi: Brian Sikulu

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mkongwe wa muziki wa Hip-Hop nchini Tanzania Chidi Benz amefunguka kuhusu albamu yake ya hivi karibuni iliyopewa jina la 'Wa2Wangu' kupata mafanikio makubwa licha ya kukosa uungaji mkono kutoka kwa wasanii wenzake.

Akizungumza katika mahojiano na Wasafi FM, Chidi Benz alisema kuwa amefurahia mapokezi ambayo video ya wimbo wake wa 'Nalia' umepata. 'Nalia' ni moja kati ya ngoma zilizomo kwenye albamu ya 'Wa2Wangu'.

Soma Pia: Nyimbo Mpya: Chidi Benz Aachia Albamu Mpya ‘Watu Wangu’

Ila alihisi kuwa hajapata uungaji mkono kutoka kwa wasanii wenzake kama jinsi alivyokuwa ametarajia. Hili lilionekana kumshangaza mno haswaa ikizingatiwa kuwa wengi wa wasanii wa bongo ashafanya kazi nao.

Alisisitiza kuwa hana kinyongo na msanii yeyote, na siku zote yeye ni msanii ambaye anawaunga mkono wanamuziki wenzake. Chidi Benz alimtaja msanii maarufu Shilole ambaye alisema kuwa amewahi kufanya kolabo na yeye, na kwenye kolabo hiyo yeye ndiye aliyeuandika wimbo mzima. Ila kwa sasa haoni Shilole akimuunga mkono kama alivyotarajia.

Alitoa pia mfano wa jinsi wasanii na watu maarufu walijitokeza kuunga mkono albamu ya staa wa muziki wa bongo Alikiba. Aidha Chidi pia alionekana kushangazwa na jinsi msanii Jux alipata uungaji mkono mkubwa wakati wa kuzindua duka lake la kuuza manguo, ilhali haoni uungaji mkono sawia kwenye albamu yake.

Msanii huyo ambaye ni mmoja kati ya wasanii wakongwe zaidi kwenye tasnia ya muziki wa Tanzania alisema kuwa yeye hana ubaya na msanii yeyote na atazidi kujituma kwani anaamini kazi yake ni nzuri.

Leave your comment