Nyimbo Mpya: Hamisa Mobetto Aachia Wimbo Mpya ‘Ex Wangu’ [Video]

[Picha: Hamisa Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki Hamisa Mobeto ameachia wimbo wake mpya wenye mahadhi ya singeli uitwao ‘Ex Wangu Remix’ akishirikiana na msanii wa singeli Seneta Kilata.

Video hiyo ambayo mpaka sasa imetazamwa takriban mara 33,000 kwenye mtandao wa Youtube imeongozwa na Creator Pro huku audio ikiwa imetayarishwa na Kenny.

Kwenye ‘Ex Wangu’ Mobetto anampa pole mpenzi wake wa zamani kwani kwa sasa ameshampata mpenzi mpya ambaye wameshibana. Kwenye aya ya kwanza ya wimbo huu Mobetto anaimba "Nakupa pole umeshachelewa, pole dear ex mwenzako nimewahiwa."

Soma: Nyimbo Mpya: Lulu Diva, Lava lava Waachia Wimbo Mpya ‘Samahani’ [Video]

Akizungumza kwenye kipindi cha Leo Tena Mobetto amesema kuwa ameamua kufanya muziki wa Singeli kwa sababu ni muziki halisi wa watanzania.

"Nimeimba singeli kwa sababu ndo ladha ya watanzania, kuna nyimbo nyingi lakini naamini kwamba mtu akisikia singeli anasema kabisa this is a sound from Tanzania," alisema msanii huyo.

Huu ni muendelezo wa wasanii kutokea nchini Tanzania kupendelea kufanya muziki kwani mpaka sasa wasanii wakubwa nchini humo kama Zuchu, Ibraah, Anjella na Lavalava wameshafanya aina hiyo ya muziki.

Aidha, Mobeto alieleza kwa kina ni kwanini aliamua kufanya remix ya wimbo huo ambao kwenye toleo halisi la wimbo huo alifanya msanii Seneta Kilata. Mobeto alisema "Kuna rafiki yangu anaitwa Ailaty yupo Oman aliipost video ya mtu anaimba, nikapenda maneno yake, yako very catchy nikamdm (Seneta Kilata) nilivyomdm palepale akarespond."

Kuhusu utofauti aliokutana nao wakati anarekodi wimbo huu wa singeli tofauti na nyimbo za kuimba, Mobetto aliongeza kwa kusema "Kwenye Singeli unatumia nguvu nyingi zaidi kuliko huku kwingine (kwenye kuimba) na unapofanya kazi na watu wanaokupa support inakuwa kuna ufadhali."

Kando na kuimba, Mobetto pia ni mwanamitindo, mfanyabiashara na muigizaji wa filamu pamoja na tamthiliya.

https://www.youtube.com/watch?v=CmSgffQYaSo&ab_channel=HamisaMobetto

Leave your comment