Biography: Mambo Matano Usiyoyajua Kuhusu Jaivah

[Image Source: Instagram]

Mwandishi: Branice Nafula

Pakua Mixes Mpya Kila Siku Ndani Ya Mdundo

Mwaka 2023 umetuletea mambo mengi sana mazuri na moja ya vitu vizuri ambavyo tasnia ya muziki Tanzania imetuletea kwa mwaka huu ni pamoja na kipaji cha aina yake kutoka maeneo ya Mburahati, Dar Es Salaam cha kuitwa Jaivah.

Kwa sasa Jaivah anatamba na ngoma yake ya Pita Kule ambayo amemshirikisha Marioo lakini miezi michache nyuma, Jaivah alitetemesha Tanzania na kibao chake cha Amapiano cha kuitwa Soup ambacho pia alifanya na Marioo, Chinno Kid, Scott London na Ks Hub.

Pamoja na kwamba watu wengi wanafahamu na kucheza nyimbo za Jaivah lakini mashabiki wengi bado hawafahamu historia na wapi alipotokea fundi huyu wa muziki wa Amapiano na ambaye kwa sasa amesainiwa kwenye mojawapo ya lebo kubwa sana nchini Tanzania, BXtra Records.

Huu hapa ni wasifu (biography) ya msanii Jaivah kutoka nchini Tanzania :

Maisha ya awali

Jaivah ambaye amezaliwa na kulelewa Mburahati, Dar Es Salaam nchini Tanzania na pia ni kaka wa mmojawapo wa watayarishaji wakubwa wa muziki nchini Tanzania, Abbah Process. 

Pamoja na kwamba watu wengi hudhani kuwa Jaivah ni msanii wa Afrika Kusini lakini fundi huyu wa muziki ana asili ya Tanzania na amesoma kwenye shule ya Seninary ya Don Bosco pindi akiwa mdogo na pia alikuwa ni mwanafunzi kwenye chuo cha biashara cha CBE.

Kuingia Kwenye Muziki

Jaivah alianza kupenda muziki udogoni baada ya kukutana na mtayarishaji wa muziki wa kuitwa Mtani ambaye aliwafundisha yeye na Abbah matumizi ya A4 ambayo nu software ya muziki.

Kutokea hapo, Jaivah alianza kufuatilia kuhusu utayarishaji wa muziki na mapenzi yake na muziki yalianzia hapo.

Ngoma Yake Ya Kwanza

Jaivah alitoa ngoma yake ya kwanza mwaka 2015 ya kuitwa Jaiva. Ngoma ya Jaiva ilipokelewa kwa ukubwa wa aina yake kwani ilimuwezesha Jaivah kutumbuiza kwenye tamasha la After Skul Bash linaloandaliwa na Clouds FM.

Jaiva pia ilifanya vizuri sana kiasi cha kupata remix kutoka kwa msanii wa rap Joh Makini pamoja na Karabani ambao kwa pamoja na Jaivah waliachia Jaiva Remix

Wasanii Aliofanya Nao Kazi

Tangu aanze shughuli zake za kimuziki, Jaivah ameshirikiana na wasanii wakubwa kutoka Tanzania ikiwemo Gigy Money kwenye Si Ulinikataa, Marioo kwenye Soup, Darassa kwenye Lock Me Down, Joh Makini kwenye Jaiva Remix na wasanii wengine wengi.

Lebo Na Aina Ya Muziki

Jaivah anafanya aina tofauti tofauti za muziku ikiwemo Hip Hop kama alivyosikika kwenye Lock Me Down, Afrobeats na kubwa kabisa Amapiano ambapo kupitia ngoma kama Soup, Yesa na Pita Kule Jaivah amedhihirisha ufundi alionao kwenye muziki huo wenye asili ya Afrika Kusini.

Kwa sasa Jaivah amesainiwa kwenye lebo ya BXtra records ambayo ina wasanii wakubwa ikiwemo Country Wizzy na Meja Kunta.  

 

Leave your comment

Top stories

More News