Ibraah Aachia Ngoma Mpya ‘Addiction’ Akimshirikisha Harmonize

[Picha: YuTube]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki Ibraah kutokea lebo ya Konde Gang ameachia ngoma mpya yenye jina ‘Addiction’ akimshirikisha Harmonize.

Kwenye ‘Addiction’, Ibraah kwa mara ya kwanza ameamua kupita kwenye mdundo wa Amapiano. 

Ibraah anazungumzia uzuri wa pombe na jinsi gani inasaidia kupunguza mawazo huku akitoa tahadhari kuhusu madhara anayoweza kupata mtu iwapo ataizidisha.

Soma pia: Ibraah Azungumzia Utata Uliotokea Konde Music Worldwide Kabla ya ‘Jipinde’ Kuachiwa

Ibraah anafungua ngoma hii kwenye aya kwanza kabisa akiisifia pombe kwa kuimba "Kwanza pombe ni dawa ukiwa na msongo wa mawazo inakuweka sawa. Pombe sio kahawa kama hauziwezi usizidishe utapagawa."

Harmonize anapokea kijiti kwenye aya ya pili ya ngoma hii ambapo “Teacher" anaeleza kinaga ubaga namna anavyojisikia baada ya yeye kunywa pombe kwa kuimba "Eeeh nikizinywa nashushia na ndumu, basi hiyo glasi naona ksma dumu. Nikizima niacheni humuhumu na usishangae nikila mhudumu."

Soma Pia: Ibraah Atangaza ujio wa Albamu yake Mpya

Mdundo wa ngoma huu umetayarishwa na Mocco Genius ambaye amehusika kutengeneza na kutayarisha ngoma za wasanii tofauti tofauti nchini Tanzania kama Zuchu, Mbosso, Diamond Platnumz na wengineo wengi.

‘Addiction’ ni muendelezo wa wasanii wa Tanzania kufanya muziki wa Amapiano na pia hata ujumbe wa ngoma hii kuhusu kusifia pombe unarandana barabara na ‘Bia Tamu’ ya Marioo pamoja na ‘Beer’ ya Benpol.

Tangu mwaka huu uanze ngoma hii ni ya tano kwa Ibraah kwani Januari mwaka huu aliachia EP yake ya ‘Karata Tatu’, kisha mwezi Agosti aliachia ‘Jipinde’ ngoma ambayo ilifanya vizuri sana Afrika Mashariki.

https://www.youtube.com/watch?v=mL3yrU792bA

Leave your comment