Ibraah Atangaza Tamasha Jipya ‘Ibraah Homecoming’

[Picha: Ibraah Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki kutokea lebo ya Konde Gang Ibraah ametangaza tamasha jipya ambalo amelipa jina la ‘Ibraah Homecoming’.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ibraah ameweka wazi kuwa tamasha hilo litafanyika huko mkoani Mtwara sehemu ambayo amezaliwa. Tamasha hiyo itafanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Soma Pia: Ibraah Azungumzia Ziara ya Muziki ya Harmonize Kulinganishwa na Ile ya Diamond

"Ni takriban mwaka mmoja sasa tangu nimeanza kufahamika kwenye kiwanda hiki cha muziki wa kizazi kipya na ndoto yangu kubwa ilikuwa ni siku moja niweze kufanya show kubwa nyumbani sehemu ambayo imenilea na kunikuza…. Hatimaye historia inaenda kuandikwa 27/11/2021 Nangwanda Sijaona Mtwara Homecoming Tafadhari naomba mnipokee" aliandika Ibraah.

Taarifa hii kutoka kwa Ibraah inakuja siku chache baada ya msanii huyo kurudi kutoka nchini Marekani ambapo aliambatana na Harmonize kwa ajili ya kwenda kufanya ziara ya kimuziki.

Soma Pia: Ibraah Afichua Sababu ya Kumwacha Harmonize Marekani na Kurudi Tanzania

Utamaduni wa wasanii wa Tanzania kurudi kufanya matamasha ya kimuziki kwenye mikoa ambayo wamezaliwa umeshamiri hasa kwa miaka ya hivi karibuni.

Zuchu alifanya tamasha lake la Zuchu Homecoming visiwani Zanzibar mwezi Agosti na kabla yake, Rayvanny alifanya tamasha lake la Homecoming Desemba mwaka 2019 kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Kwa sasa, macho na masikio ya mashabiki yapo kwenye himaya ya Konde Gang kwa ajili ya tamasha hilo la Ibraah, ambaye pia aliujulisha umma kuwa albamu yake iko tayari na ni suala la muda tu mpaka itakapoingia sokoni.

Leave your comment