TANZANIA: Je Naj ageuka kuwa mkalimani wa Baraka da Prince?!!

 

 

 

Barakah Da Prince yupo nchini Afrika Kusini alikoenda kufanya mambo mengi ikiwemo kushoot video mpya na pia ziara kwenye vyombo vya habari. Amezunguka kwenye vituo vya redio kadhaa na pia kuhojiwa na kituo cha MTV Base.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, kituo hicho kiliweka video fupi inayomuonesha mtangazaji akimhoji Barakah na huku pembeni akiwa na mpenzi wake, Naj. Mtangazaji huyo anauliza maswali kwa Kiingereza, Naj anamtafsiria Barakah anayejibu kwa Kiswahili na Naj anamtafsiria mtangazaji na mchakato unaonekana kuendelea hivyo katika interview nzima.

Post hiyo imepata comments zaidi ya 240 na wengi waliochangia ni watanzania. Mitazamo ni tofauti, wapo wanaombeza staa huyo kwa kutojua Kiingereza, wapo wanaomsifia kwa kukitangaza Kiswahili na wapo wanaompa moyo.

Ukweli ni kwamba Kiingereza kwa wasanii wengi wa Tanzania limekuwa janga kubwa na sio kosa lao kabisa. Kuna sababu kubwa mbili. Kwanza, wasanii wengi wa Bongo Flava wameingia kwenye muziki kama ajira yao baada ya kukosa elimu ambayo ingewasaidia kuwa na ajira za kawaida.

Wengi wameishia kidato cha nne, wengi darasa la saba na wengine hawakumaliza kabisa sekondari kutokana na kukosa fedha za kujisomesha. Ni wachache sana ambao wamesoma hadi kidato cha sita au kupata stashahada au shahada. Muziki ambao hauhitaji Kiingereza kuumudu, ukawa mkombozi wao.

Mfano mzuri ni Diamond ambaye naye alipitia njia hii hii ya kuadhirika, kusimangwa na kukosa raha kila alipokuwa akihitajika kuhojiwa kwa Kiingereza. Yeye pia alitumia wakalimani na aliwahi kukiri jinsi kutokujua Kiingereza kulivyomtesa.

Alichukua hatua na kuamua kujifunza Kiingereza huku pia wapenzi wake wa zamani wakiwemo Wema Sepetu na Penny wakimsaidia. Leo hii Diamond anaongea Kiingereza vizuri kabisa.

Pili, mfumo wa elimu ya Tanzania una udhaifu mkubwa katika kumjenga mwanafunzi kukijua Kimombo. Elimu yetu inawafanya hata wanafunzi wa chuo kikuu kuwa na Kiingereza cha kubabaisha, sembuse mtu aliyeishia darasa la saba au kidato cha nne?

 

 

Sina uhakika na elimu ya Barakah Da Prince lakini naamini ni ya kawaida sana ambayo inamwacha katika wakati mgumu kuweza kujieleza kwa Kiingereza kama walivyo watanzania wengi. Ni sahihi kabisa kuamua kumtumia mpenzi wake Naj kama mkalimani na kumpa uhuru wa kujieleza vizuri kwa lugha anayoifahamu.

Kama akisema ajilazimishe aongee hicho hicho cha kubabaisha, ataaibika zaidi na pia kushindwa kutoa maelezo anayodhamiria kuyatoa.

Bahati nzuri ni kwamba yupo chini ya label makini, Rockstar4000 ambayo chini ya msomi kama Seven Mosha, nina uhakika suala la kumtafutia mwalimu wa Kiingereza wamelifikiria. Barakah ana bahati ya hata kufika hapo alipofika ndani ya muda mfupi na kuna kila dalili kuwa akuwa Alikiba au Diamond ajaye, hivyo ni vyema akajiandaa kuwa mwanamuziki wa kimataifa.

Na ukiwa mwanamuziki wa kimataifa, huna budi kukifanya Kiingereza kuwa rafiki yako wa karibu. Barakah asiumizwe na kejeli za baadhi ya watanzania ambao ninaamini wengi wao nao Kimombo kimewapita kushoto, bali achukue kama changamoto ya kuongeza hasira kujifunza zaidi. Akiweza kujieleza kwa lugha hiyo ataweza kufanya interview kwa kujiachia, kuchangamka na kufurahia zaidi.

 

 

Chanzo: Bongo5

 

Pakua app ya Mdundo sasa: smarturl.it/mdundo_ig_play_tz

 

 

Leave your comment