TANZANIA: Msanii Fid Q Aitumia Ombi Serikali

Msanii wa muziki wa Hip Hop Bongo, Fareed Kubanda maarufu kama Fid Q, amewasilisha ombi la kutaka kutambuliwa na kuundiwa sera yake kwa sanaa ya muziki Bongo ili iweze kujitegemea.

Fid Q ametumia siku ya Wafanyakazi kutoa ombi hilo kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ikiwa ni siku moja tu tangu ateuliwe na Chama cha Muziki wa Kizazi Kipya Tanzania (TUMA), kuwa Mwenyekiti wa kamati ya Fedha, Mipango na Uchumi.

"SANAA ni sekta rasmi hivi sasa lakini bado haijapewa sera na hiyo ni sawa na kuwa na ofisi isiyokua na KANUNI, TARATIBU wala SHERIA. Kwa ufupi bado tunaongozwa na sera ya utamaduni. Tunayofuraha kubwa ya kuitumia sikukuu hii ya wafanyakazi kwa kuikumbusha WIZARA na SERIKALI kwa ujumla kutuundia sera ili SANAA yetu iweze kuleta tija kwenye jamii. (Na katika hilo tunashauri RASIMU iandaliwe na WASANII wenyewe)." ameandika.

Aidha Fid Q ameongeza kwa kusema wasanii wanalipa kodi kwa kazi zao za sanaa lakini kazi zao hazilindwi na serikali, kitu ambacho kinatishia usalama wa wao kuendelea kulipa kodi siku za usoni kwani hawatakuwa wanatengeneza faida.

Fid Q ameteuliwa hivi karibuni na TUMA kushika nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa kamati ya Fedha, Mipango na Uchumi wa chama hicho, ambapo ameanza kazi rasmi jana April 30.

Courtesy: eatv.v

Leave your comment