TANZANIA: Joh Makini Afunguka Juu ya Kupangiwa Mashairi

Rapa kutoka Weusi anayetamba kwa sasa na 'hit song' ya 'Mipaka', Joh Makini amefunguka na kudai hawezi kupangiwa aina ya mashairi ya kuimba katika muziki wake kwa kuwa hicho ndio kitu pekee kinachoweza kumtofautisha yeye na wasanii wengine nchini.

Joh Makini ameeleza hayo kupitia kipindi cha eNewz kutoka EATV baada ya kupita upepo wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) kufungia baadhi ya kazi za wasanii zilizokuwa hazina maadili huku wengine wakitakiwa kubadilisha baadhi ya mashairi yaliyokuwepo katika nyimbo zao ili mradi zilete maana nzuri katika jamii ya kitanzania ambao ndio wasikilizaji wao.

"Tunavyoandika mashairi wakati mwingine unakuwa tofauti na watu wanavyopokea kitaani kwa hiyo ikawa sisi tunatoa nyimbo yeye maana fulani halafu wao BASATA wakasikiliza huo wimbo wakasema wanaufungia huo wimbo kwasababu unamaana mbaya wakati wewe hukumaanisha hivyo", amesema Joh Makini.

Pamoja na hayo, Joh Makini ameendelea kwa kusema "mimi nafikiri sio kitu cha kukurupuka kama haya matukio yalivyokuja hivi ghafla, ni kitu cha kukaa chini pande zote mbili ili watu waweze kuelewana na kubaliana kuwa sasa hivi njia ni hii kwasababu kesho hatuwezi kujua ni wimbo gani utafungiwa na wala huwezi kujua sababu zake. Huwezi kunipangia mashairi ya kuimba maana ukinizuia mimi kuacha kuandika jinsi ninavyoandika maana yake umeshanizuia niache sanaa kwasababu hicho ninachoandika ndiyo sanaa iliyopo ndani yako na ndicho kinanitofautisha na wengine".

Courtesy of eatv.tv

Leave your comment