TANZANIA: Aslay na Nandy Kupelekwa Mahakamani

Wasanii wa kizazi kipya Aslay pamoja na mwanadada Nandy wanaoendelea kufanya vizuri na kibao chao cha 'Subalkheri Mpenzi' wanatarajiwa kuburuzwa Mahakamani kutoka na kuimba wimbo huo bila ya ridhaa ya wahusika.

Hayo yameibuka baada ya mmiliki wa wimbo huo, Kikundi cha Tarab Asilia visiwani Zanzibar (Culture Music Club) kudai pesa zilizotolewa jumla ya Tsh. 800,000 kama fidia za kutumia kazi hiyo hawazitambui hivyo wanajipanga kuwapeleka mbele ya Mahakama.

Akizungumza Katibu Mtendaji wa kikundi hicho, Taimur Rukuni Twaha, amesema wasanii hao kabla ya kuimba tena upya wimbo huo walipaswa kuonana na uongozi huo ili kukubaliana jambo ambalo hawakufanya hivyo.

"Walichokifanya Aslay na Nandy kwenda kwa waimbaji wetu na kuwapa kiwango hicho cha fedha kwetu tunaona hakikubaliki na wametoa kama zawadi tu kwa sababu thamani ya wimbo wetu haulingani na kiwango hicho. Kwa mujibu wa katiba ya kikundi chetu, ibara ya sita inaeleza nyimbo zote zilizoimbwa na kikundi ni mali ya kikundi na kwamba muimbaji, mtunzi na muweka sauti watakuwa na haki zao kupitia kikundi hicho", amesema Twaha.

Kwa upande mwingine, Twaha amesema msimamo wao utabaki pale pale wa kuwafikisha Mahakamani wasanii hao endapo watashindwa kutimiza masharti waliyopewa na uongozi wa kikundi hicho.

Chanzo: Nipashe

Leave your comment