TANZANIA: G Nako Akosoa Wanaojadili Changamoto za Muziki

Msanii G Nako kutoka 'Weusi' amewataka wasanii na watu wanaohitaji kuwekeza na kufanya biashara ya muziki wasiogope changamoto zilizomo, bali fursa na uwezo wao wa kuzikabili, huku akiwakosoa wanaweka changamoto hizo hadharani.

G Nako ambaye alikuwa katika 'Dakika Kumi za Maangamizi' kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio amesema kwenye kila kazi kuna changamoto nyingi lakini kuziongelea kwenye vyombo vya habari ni kuwakatisha tamaa wale wachanga wanaotaka kuinuka na kuwazuia kuonesha uwezo wao.

“Hakuna kazi isyokuwa na changamoto lakini kuzisema hadharani ni kuwakatisha tamaa wasanii wachanga wanaotamani kufanya kama mimi au wanaonitazama mimi,mimi nawashauri kama kuna mtu anapenda kufanya hii biashara au kuwekeza kwenye muziki asisikilize maneno ya watu kwa sababu yatakukatisha tamaa ya kujaribu” - Gnako

Katika hatua nyingine G Nako amesema muziki anaoufanya ni muziki wa ukombozi hivyo kila mtu huwa anawasilisha mawazo kwa mtindo ambao ana uwezo nao na kusisitiza kuwa ukombozi unadaiwa siyo kuombwa.

Aidha ameongeza kuwa kundi lake la Nako 2 Nako bado lipo halijavunjika kama jinsi wengi wanayofikiria na tayari wana nyimbo zisizopungua tano zinasubiri kuachiwa.

"Nako 2 nako tupo hata kazi tulizofanya nazo zipo, tuna kazi kama sita tumeshatengeneza hapa ikitokea project tunaweza kufanya albam, tatizo linakuja tu kwamba mimi nafanya 'movement' zangu kivyangu na wenzangu vivyo hivyo, muziki ni biashara mwisho wa siku studio unalipa, matangazo na mengineyo kusipokuwa na usimamizi ni hasara,sisi bado hatujapata mtu wa kusimamia kazi”. G Nako

Source: eatv.tv

 

Leave your comment